Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni 208 ili zitumike kujenga shule mpya za sekondari kwenye Halmashauri zote hapa nchini ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani.
Hayo yamesemwa leo (Jumamosi, Julai 8, 2023) na Naibu Waziri (OR-TAMISEMI), Deogratius Ndejembi alipopewa nafasi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa awasalimie wananchi na watumishi wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini kwenye kijiji cha Mkunwa, wilayani Mtwara, mkoani Mtwara.
“Halmashauri zote nchini, ziko 184 zimepatiwa kati ya sh. milioni 570 na milioni 600 za ujenzi wa shule mpya za sekondari. Tumewapa Wakurugenzi hadi Novemba, mwaka huu wawe wamekamilisha ujenzi huo ili waweze kupokea wanafunzi ifikapo Januari, 2024.”
Akizungumza na wananchi hao na watumishi mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua kuwa Halmashauri hiyo ni changa na ndiyo maana inapeleka fedha ili kuwawezesha watumishi hao watimize majukumu yao.
Amewataka Wakala wa Majngo nchini (TBA) ambao ni wakandarasi wa mradi huo, wakamilishe majengo kwa haraka ili wananchi waanze kupata huduma. “Wananchi wanataraji kuona haya majengo yakikamilika. Kwa hiyo tumieni mbinu ya kujenga usiku na mchana ili yakamilike mapema,” amesisitiza.
Amewataka Mkuu wa Wilaya ya Mtwara na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, wakae na TBA na NHC ili waandae mradi wa kujenga nyumba za watumishi. “Tunataka haya yafanyike ili tukamilishe uwepo wa makao makuu ya Halmashauri yenu,” amesema.
Akiwa njiani kuelekea Nanyamba, Waziri Mkuu alisimama kata ya Nanguruwe na kuzungumza na wananchi wa kata hiyo na kujibu masuala kadhaa yaliyoibuliwa na wananchi hao. Masuala hayo yalihusu maji, umeme, shule ya kidato cha tano na changamoto ya tiba ya moyo kwa mtoto Zahir Akili mwenye mwaka mmoja na miezi mitano.
Akitoa ufafanuzi wa tatizo la maji, Meneja wa RUWASA mkoa wa Mtwara, Mhandisi Primy Damas alisema Serikali imesaini mkataba wa sh. bilioni 5.7 wa kutoa maji Nanyamba hadi Nanguruwe ambao unatarajiwa kuanza kujengwa Julai, mwishoni. “Mradi huu ni wa miezi 12, ulisainiwa siku tatu zilizopita na mkandarasi tayari ameshapewa kazi,” amesema.
Mbali na mradi huo, Mhandisi Damas alisema wameshachimba kisima kwenye hospitali ya Halmashauri iliyopo Nanguruwe na wanatarajia kufunga pampu ili wakabidhi kisima hicho. “Pia tunatarajia kujenga vizimba viwili nje ya hospitali ili visaidie kutoa maji kwa wananchi.”
Kuhusu shule ya kidato cha tano, Waziri Mkuu alisema suala hilo liko mikononi mwao na Madiwani kupitia vikao vyao wanaweza kuamua ijengwe mpya au kuchagua shule mojawapo na kuipandisha hadhi iwe ya kidato cha tano na sita.
Kuhusu tatizo la moyo la mtoto Zahir, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Hamad Nyembea asimamie maandalizi ya mtoto huyo na mama yake kupelekwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili afanyiwe uchunguzi zaidi. “Tiba ya moyo kama hiyo inagharimu sh. milioni 28, na huyu mama hana huo uwezo. Serikali itagharimia matibabu ya mtoto huyo.”
Awali, mama yake Zahir, Bi. Aisha Luyenda alisema mtoto wake alibainika kuwa na tatizo la moyo kuelekea upande wa kulia wa kifua badala ya kushoto (dextrocardia) na kwamba anahitaji matibabu makubwa zaidi lakini hana uwezo.
Waziri Mkuu alikagua pia shule ya Sekondari Dinyecha na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika shule ya msingi Nanyamba.
(mwisho)