Home Kitaifa ZAIDI YA MILIONI 200 ZATUMIKA KUKARABATI HOSPITALI YA BOMBO

ZAIDI YA MILIONI 200 ZATUMIKA KUKARABATI HOSPITALI YA BOMBO

Na. WAF – TANGA

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa zaidi ya Shilingi milioni 200 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya Afya katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa-Bombo,Tanga.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Jonathan Budenu wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma za afya na utekelezaji wa miradi ya afya katika mkoa huo chini ya ufadhili wa fedha za Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya maboresho ya Miundombinu ya kutolea huduma hizo.

Pamoja na maboresho mengine fedha hizo zimetumika katika kukarabati jengo la wagonjwa mahututi (ICU) ambalo tayari limeshaanza kutoa huduma kwa wagonjwa pamoja na ukarabati wa jengo la Huduma za Dharura (Emergence Department).

Dkt. Budenu amesema ukarabati wa majengo hayo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali ambapo wagonjwa walilazimika kusubiri kukamilika shughuli nyingine ambazo zilikuwa zikitegemea chumba hicho kabla ya wao kupatiwa huduma.

Amesema huduma katika Jengo la Huduma za Dharura zinatarajiwa kuanza katikati ya mwezi Julai mwaka huu.

Akizungumzia hali ya Utoaji huduma za Afya katika Mkoa wa Tanga Dkt. Budenu ameishukuru Serikali kwa kujenga Hospitali Mpya 5 ambapo tayari Hospitali 3 zilizopo Muheza, Korogwe na Tanga Jiji tayari zimeshaanza kutoa Huduma huku Hospitali ya Handeni ikitarajia kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi Julai na ile ya Kilindi ikitarajiwa kuanza kutoa huduma mwezi Agost mwaka huu.

Serikali pia imejenga vituo vya Afya 17 Mkoani humo ambapo vituo 7 kati ya hivyo vinatarajiwa kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.

Vilevile Dkt. Budenu akiishukuru Serikali kwa kusaidia kukabiliana na changamoto ya watumishi na kupitia ajira mpya zilizotolewa na Serikali watumishi wapya 200 wamepelekwa mkoani humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!