Home Kitaifa WIZARA YA MAJI YAMKUBALIA MATHAYO KUFIKISHA MAJI KWA ASILIMIA 100 JIMBO LA...

WIZARA YA MAJI YAMKUBALIA MATHAYO KUFIKISHA MAJI KWA ASILIMIA 100 JIMBO LA MUSOMA MJINI

Na Shomari Binda-Musoma

WIZARA ya Maji imekubali ombi la mbunge wa jimbo la Musoma mjini kutoa kiasi cha shilingi milioni 309 kukamilisha kufikisha maji kwenye maeneo yote ya jimbo.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,mhandisi Cyprian Luhemeja,wakati akijibu maombi ya mbunge huyo kwenye kikao kilichowashirikisha watumishi wa wizara hiyo mkoa wa Mara.

Amesema amefanya ziara mkoa mzima wa Mara na kuona hali ya upatikanaji wa maji ni mzuri na changamoto ndogo zilizopo zinafanyiwa kazi.

Luhemeja amesema maji ni huduma muhimu hivyo wananchi wote watafikiwa na kupata maji safi na salama na kumshukuru mbunge Mathayo kwa kuwa karibu na watumishi.

Amesema mbunge wa jimbo la Musoma mjini ameomba kiasi cha milioni 309 tutakwenda kukaa ofisini na kuzileta ili asiwe na tatizo la maji tena.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 maeneo yote nchini yanafikiwa na huduma ya maji.

Akizungumza na watumishi wa mamlaka za maji mkoa wa Mara amewataka kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuwafikishia wananchi huduma ya maji.

Amesema huduma nzuri kwa wateja ni jambo muhimu ikiwa ni pamoja na kuzalisha maji ya kutosha na kukusanya mapato ili kuongeza kipato.

Tukikusanya mapato ya kutosha na kufanya kazi kwa bidii na hata mishahara yetu itakuwa mikubwa hivyo tujitahidi kufanya kazi” amesema Luhemeja.

Akizungumza kwenye kikao hicho mara baada ya kutembelea miradi ya maji jimbo la Musoma mjini na maeneo yatakayofikishiwa maji,mbunge wa jimbo la Musoma mjini,Vedastus Mathayo,ametoa shukrani kwa wizara ya maji.

Amesema Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) inafanya kazi nzuri katika kufikisha huduma ya maji kwa wananchi ambayo inapaswa kuungwa mkono.

Mathayo amesema zikipatikana milioni 309 jimbo la Musoma mjini litafikiwa na huduma ya maji kwa asilimia 100 na wananchi kuendelea na maisha mengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!