Home Kitaifa WIZARA YA MADINI YAFANYA MKUTANO WA PILI KWA KUWAPA WACHIMBAJI WAKUBWA, WA...

WIZARA YA MADINI YAFANYA MKUTANO WA PILI KWA KUWAPA WACHIMBAJI WAKUBWA, WA KATI MWELEKEO WA WIZARA

Ikiwa ni Jitihada za Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kiuwekezaji katika Sekta ya Madini nchini, Wizara ya Madini na Chemba ya Migodi zimekutana Oktoba 27, 2023, ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu uliowekwa na Wizara kukutana na Wachimbaji Wakubwa, wa Kati na Watoa huduma migodini kila Robo ya Mwaka kupitia Chemba ya Migodi.

Mkutano huo ni wa Pili kufanyika baada ya mkutano wa kwanza uliofanyika mapema mwezi Julai, 2023, yote ikilenga kuleta ukaribu kati ya serikali na wadau wa sekta ya madini pamoja na kujadili kwa pamoja changamoto ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyozuia utekelezaji wa miradi, shughuli na biashara ya madini nchini.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ambaye amekutana na wadau hao kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Madini, amesema, mikutano hiyo inatumika kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa miradi wanayoisimamia ili kuchochea uwekezaji.

‘’Tukiondoa vikwazo itasaidia kuongeza shughuli za uchimbaji nchini na hatimaye tutaongeza uchumi na mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, tutaongeza ajira, maendeleo ya nchi na watu. Chukulia mfano wa Mkoa wa Geita tu, Serikali inakusanya shilingi bilioni 243, tunataka shughuli za madini zifanyike mikoa yote katika mazingira rafiki,’’ amesisitiza Mavunde.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amefungua mlango kwa wawekezaji wote nchini na kueleza kuwa hategemei kuwa kikwazo kwao na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali kuendeleza Sekta ya Madini nchini.

‘’Kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Uwekezaji Sekta ya Madini nilisema moja ya vitu nisivyovipenda ni urasimu. Nipo hapa kuondoa urasimu nitafanya kazi na ninyi na tutashirikiana vizuri, ‘’ amesema Waziri Mavunde.

Aidha, ametumia jukwaa hilo kuwapongeza na kuwashukuru wadau hao na kueleza kuwa, kwa pamoja wamewezesha kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 9.1 katika Mwaka wa Fedha 2022/23.

Waziri Mavunde ameendelea kuwasisitiza kuhusu dhamira ya Serikali kutekeleza Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri ambapo amesema Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST) inalenga kufanya tafiti za kina kwa kutumia ndege ili kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 kutoka asilimia 16 ya sasa. Tunatakakwenda kwenye uchumi wa madini mkakati. Tanzania ina utajiri wa kutosha wa madini mkakati na kwa kuzingatia mahitaji ya dunia ya tani milioni 150 ya madini hayo ifikapo mwaka 2050 ni lazima ijipange kunufaika ipasavyo kiuchumi,’’ amesema Mhe. Mavunde.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Mhandisi Philbert Rweyemamu amesema kuwa lengo la mikutano hiyo ni kujadili na kujenga uelewa wa pamoja katika masuala mbalimbali hususan masuala yanayohusu mifumo ya Kisheria na Kisera na kuongeza kwamba, mikutano hiyo inalenga kuiwezesha sekta ya madini kuendelea kufanya vizuri.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema utaratibu huu unawezesha serikali kupata mrejesho na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowasilishwa na wadau na kueleza kuwa, lengo la serikali ni kuwawezesha wadau kutekeleza majukumu yao vizuri kupata faida na serikali kunufaika kupitia rasilimali madini.

‘’Tayari Wizara imeweka utaratibu kuwa na focal point katika kila miradi inayotekelezwa ili kuwawezesha wadau kufanya kazi zao kwa muda uliopangwa na serikali kupata mrejesho wa haraka,’’ amesisitiza

Aidha, katika mkutano huo, Wizara imetoa mrejesho wa yale yaliyojadiliwa katika mkutano uliopita.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao wamepongeza utaratibu wa kukutana na kujadili kwa pamoja na baadhi kupendekeza taasisi nyingine za umma zinazohusika na masuala ya madini moja kwamoja kushirikishwa katika mikutano hiyo ili kuendelea kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya madini.

Mbali na wanachama wa Chemba ya Migodi, mkutano huo umehudhuriwa na watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Australia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!