Wataalam wa Wizara ya Madini wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo pamoja na Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga wamefanya mazungumzo na ujumbe wa Kampuni ya Perseus Mining Limited kutoka nchini Australia ambayo inatarajia kuwekeza kwenye Mradi wa Uchimbaji Mkubwa wa Madini Dhahabu wa Nyanzaga uliopo Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza.
Katika kikao hicho kilichofanyika leo Januari 15, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Madini Mtumba Jijini Dodoma pamoja na mambo mengine, kimejadili masuala kadhaa ili kuharakisha uwekezaji huo. Masuala hayo ni pamoja na Kodi, Mrabaha, Tozo za Uagizaji bidhaa, pamoja na mfumo wa Fedha wa Kampuni hiyo.
Kikao hicho ni mwendelezo wa kikao kilichofanyika Januari 7, 2024 jijini Dodoma kati ya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde na Wataalam kutoka Wizara ya Madini pamoja na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni hiyo ya Perseus Mining Limited Jeffrey Quartermaine.