Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali leo Novemba 3, 2023 ameongoza taasisi zinazofungamana katika shughuli za uchimbaji sambamba na wawekezaji ili kujadili changamoto za ikolojia katika maeneo ya uchimbaji.
Hayo yamejiri katika kikao cha pamoja kilichofanyika jijini Dar es Salaam kilicholenga kupata uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa kila sekta zinazohusika katika usimamizi wa sheria katika shughuli za uchimbaji madini
Akizungumza katika kikao hicho, katibu Mkuu amesema Serikali ipo makini kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuhakikisha wanafanya uchimbaji unaofuata sheria za nchi ili kuongeza pato la Taifa na kuwanufaisha wananchi.
Katibu Mkuu Mahimbali amewataka wataalamu katika sekta mbalimbali zinazohusika na kutoa vibali kwa wawekezaji wa madini kutekeleza majukumu yao na kuharakisha michakato ya upatikanaji wa Vibali hivyo ili kuruhusu shughuli za uchimbaji kuendelea.
Aidha, wataalamu wamejadili kwa pamoja umuhimu wa kufanyika kwa Tathimini ya Kimazingira ya Kimkakati (SEA) katika maeneo yote yanayohusisha miradi mingine zikiwemo shughuli za uchimbaji ili kulinda ikolojia ya eneo husika.
Kikao hicho cha pamoja kimekwenda sambamba na wasilisho la maendeleo ya mradi kutoka kampuni ya MANTRA yenye leseni ya Uchimbaji wa Madini ya Uranium katika mto Mkuji Wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma na kuahidi kufuata sheria na matakwa ya Serikali katika kuendeleza mradi huo.
Kikao hicho kimehusisha wataalamu kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Taasisi ya Utafiti na Jiolojia, Wizara ya Maliasili, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Nyumba na Makazi, Wizara ya Maji, Wizara ya Nishati TANAPA, Mamlaka ya Wanyama Pori (TAWA), TAWIRI, NEMC na TANESCO.