Home Kitaifa Wilaya ya Serengeti ilivyojipanga na mikakati ya kilimo nchini kuunga mkono serikali

Wilaya ya Serengeti ilivyojipanga na mikakati ya kilimo nchini kuunga mkono serikali

Na Shomari Binda

MWAKA 1975 akiwa mkoani Tabora, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akizungumza na viongozi wa mkoa huo alisisitiza suala la umuhimu wa mashamba darasa.

Serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwaondoa wakulima kwenye umasikini kwa kuja na mipango mbalimbali ya kuboresha sekta ya kilimo.

Moja ya mipango ni ule wa miaka 5 wa uhimilivu wa chakula na kuondokana na umasikini ambao ushirikisha pia mataifa mengine ya Afrika.

Licha ya mipango huo upo pia ule wa “BBT” (Jenga Kesho iliyo Bora) unaolenga kuwapa vijana mafunzo ambayo yatawawezesha kufanya kilimo chenye manufaa ya kiuchumi.

Haya yote yanafanyika kuleta mabadiliko kwenye sekta ya kilimo hapa nchini ikiwa ni pamoja kukifanya kuwa sehemu ya kukuza uchumi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akijibu sehemu ya maswali ya vijana wanaojishughulisha na kilimo jijini Dar es salam alisema maji yaliyopo baharini na kwenye maziwa ni vyema yakatumika kunufaisha kilimo.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliwahi kusema ardhi asilimia 65 bado haijatumika na inatakiwa kutumika kwenye kilimo kwaajili ya kuzalisha chakula kitakachotosheleza nchi na kingine kuuzwa nje ya nchi.

Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kama moja ya wilaya za kimkakati imejipanga kuendana na kasi hii ya mabadiliko kwenye sekta ya kilimo hapa nchini.

Hivi karibuni kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauti hiyo licha ya mambo mengi yaliyojadiliwa ni pamoja na kuanzisha mashamba darasa kwenye Kata zote 30 za halmashauri hiyo.

Mashamba darasa hayo lengo lake ni wakulima kujifunza kilimo chenye tija na kuweza kufikia malengo ya kuwainua kiuchumi kupitia kilimo

Huu ni mpango mzuri ambao halmashauri ya Serengeti umekuja nao na kama utasimamiwa vizuri na maafisa ugani na viongozi wengine kwenye Kata husika.

Kwenye kikao hicho cha baraza la madiwani, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bwenda Bainga,ambaye ni Afisa Kilimo na Mifugo alibainisha namna mpango huo utakavyosimamiwa.

Bainga aliwaeleza madiwani namna watakavyo wasimamia wataalam na viongozi kuanzisha mashamba darasa na kuyasimamia ili wananchi kujifunza.

“Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kwenye sekta ya kilimo ambazo tunaziona kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hasssn”

“Waheshimiwa madiwani na sisi kama halmashauri ni muhimu kuunga mkono juhudi hizi kama halmashauri ya Serengeti kwa kuanzisha mashamba darasa” ,alisema Bainga.

Wazo hili la kuanzishwa kwa mashamba darasa kwenye halmashauri ya wilaya ya Serengeti lilipokelewa na madiwani na kudai ni mpango wenye malengo mazuri.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Samson Ryoba alisema wamepokea kwa mikono miwili mpango huo wa mashamba darasa.

Alisema wakulima wanahitaji kupata elimu ili kuweza kufanya kilimo chenye tija na kuinuka kiuchumi kupitia kilimo wanachokifanya.

Ryoba alisema kama madiwani licha ya kupokea mpango huo watakwenda kuusimamia kwenye Kata zote 30 ili wakulima wajifunze kupitia mashamba hayo.

Makamu Mwenyekiti huyo alidai juhudi kubwa za serikali kwenye sekta ya kilimo zinapaswa kuungwa mkono ili malengo ya nchi yaweze kutimia.

Mpango huu wa uanzishwaji wa mashamba darasa kwenye Kata 30 za halmashauri ya Wilaya ya Serengeti unapaswa kupongezwa kwa kuwa una nia njema kwa wakulima.

Wakati serikali ikiendelea na mikakati mizuri kwenye sekta ya kilimo hapa nchini,halmashauri, wilaya na mikoa hapa nchini zisibaki nyuma bali ziende kwa pamoja.

Kwa mkoa wa Mara yapo maeneo makubwa kwa shughuli za kilimo na kama yatasimamiwa vizuri na mipango iliyopo ya serikali itasaidia kuinua uchumi kupitia kilimo.

Jukwaa la Mfumo wa Chakula liliofanyika hapa nchini na kuwashirikisha wakuu wa wilaya,mikoa na viongozi mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi lishuke hadi kwenye Kata na vijiji ili kuwafikia wakulima.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba-0755487117.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!