Home Kitaifa WAZIRI UMMY: JUKUMU LETU NI KUHAKIKISHA MGENI ANAYEINGIA NCHINI HALETI MAAMBUKIZI

WAZIRI UMMY: JUKUMU LETU NI KUHAKIKISHA MGENI ANAYEINGIA NCHINI HALETI MAAMBUKIZI

Na.Catherine Sungura,WAF, Kyerwa

Jukumu la Wizara ya Afya ni kuhakikisha yeyote anayeingia nchini Tanzania haingizi ugonjwa kutokana na muingiliano baina ya wananchi wa Tanzania na nchi za jirani ikiwemo nchi ya Uganda.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 5/10/2022 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea mpaka wa Murongo uliopo Wilayani Kyerwa Mkoani Kagera.

Waziri Ummy amesema kuwa wilaya hiyo yenye kata 24 na kati ya kata hizo, kata 12 zinapakana na nchi jirani ya Uganda na Rwanda hivyo Serikali inaendelea kuimarisha njia zote za kujikinga ili kuzuia magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Ebola.

Tumejionea hapa wana muingiliano wa pande zote mbili ambapo hapa kuna soko kubwa la ndizi na kwa siku wanaingia watu zaidi ya 200 hivyo jukumu letu kama Wizara ya Afya ni kuhakikisha yeyote anayeingia nchini haleti maambukizi au hana maambukizi.” Amesema Waziri Ummy.

Ameendelea kusema, Wizara haitosubiri kuwapima tu joto wanaoingia nchini kupitia mipakani bali inaenda kuwekeza zaidi katika kutoa elimu kwa jamii ili mtu aonapo dalili afanye nini na njia zipi za kujikinga.

Aidha, Waziri Ummy ameridhishwa na utayari wa kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola katika Wilaya ya Kyerwa kwa kuchukua tahadhari ambapo toka tarehe 20/9/2022 hadi leo wameweza kuwapima wamanchi 6000 wanaoingia nchini Tanzania pamoja na madereva wa magari wapatao 500.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe.Rashid Mwahimu amesema, Wilaya yake imejipanga kudhibiti tishio la ugonjwa wa Ebola kwa kuwaelimisha viongozi wa vitongoji kusajili wageni wote wanaoingia kwenye vijiji vyao ili kulinda usalama kwani wilaya hiyo ina mipaka isiyo rasmi ipatayo thelathini.

Vilevile Mhe. Rashid Mwahimu ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuwapatia vifaa kinga vya kukabiliana na ugonjwa huo kwa watoa huduma za afya wilayani hapo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!