Home Afya WAZIRI UMMY AFIKA KWENYE VIJIJI UGONJWA WA MARBURG ULIPOANZIA

WAZIRI UMMY AFIKA KWENYE VIJIJI UGONJWA WA MARBURG ULIPOANZIA

Na. WAF – Bukoba, Kagera

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kutembelea vijiji vya Kata ya Maruku na Kanyangele vilivyopo Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera kwa lengo la kujionea hali inavyoendelea baada ya kutangazwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg Mkoani humo.

Katika Ziara hiyo, Waziri Ummy ameambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Zabron Yoti pamoja na Mwakilishi wa Shirika la UNICEF Tanzania Bi. Shalini Bahuguna ili nao wajionee hali ya ugonjwa huo inavyoendelea kudhibitiwa nchini Tanzania.

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa sasa hali ni salama na kuwataka Wananchi wa vijiji hivyo, wana Kagera na watanzania kwa ujumla kuondoa hofu na kuendelea na shughuli zao kwa kuwa Serikali inawajali Wananchi wake.

Niwatoe hofu Watanzania tuendelee kufanya kazi zetu lakini tuzingatie maelekezo ya Serikali ya kujikinga na ugonjwa huu kwa kuepuka kushikana mikono hususan kipindi hiki lakini pia tujitahidi kunawa mikono mara kwa mara na maji tiririka kwa sabuni.” amesema Waziri Ummy

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na juhudi za kuhakikisha ugonjwa huo unamalizika kwa haraka na hautatokea tena katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kanyangele Bw. Hamim Hassan ameishukuru Serikali kwa kufanya juhudi kubwa ambapo hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeongezeka kuwa na ugonjwa huo.

Hatua za haraka za Serikali kupitia Wizara ya Afya zilizochukuliwa za kuwaweka sehemu maalumu waliokuwa karibu na wagonjwa imesaidia sana kutoendeleza maambukizi kwengine na hali ni shwari kwa sasa.” amesema Bw. Hassan

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!