Home Michezo WAZIRI SIMBACHAWENE AWAPA KONGOLE TIMU ZA MICHEZO OFISI YA WAZIRI MKUU

WAZIRI SIMBACHAWENE AWAPA KONGOLE TIMU ZA MICHEZO OFISI YA WAZIRI MKUU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe: George Simbachawene amezipongeza timu za michezo za ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushiriki na kupata ushindi wakati wa mashindano ya michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) ilifanyika Mkoani Tanga .

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) Mhe. George Simbachawene akizungumza baada ya  kukabidhiwa vikombe Viwili  vya ushindi kutoka kwa washiriki wa Ofisi ya Waziri Mkuu walioshiriki katika Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yaliyofanyika Mkoani Tanga.

Ametoa pongezi hizo mara baada ya kupokea vikombe viwili kutoka kwa wanamichezo walioshiriki kwenye michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba wanawake na wanaume, draft, mpira wa miguu, mbio za baiskeli na riadha.

Waziri alitumia fursa hiyo kuwaasa wanamichezo wa ofisi hiyo kuongeza kasi kwenye kushiriki michezo licha ya michezo kuwa ni ajira kwa wanamichezo wengine lakini pia inaleta afya na kujenga mahusino mazuri baina ya wanamichezo hivyo anaamini itaongeza ufanisi zaidi katika ufanyaji kazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) Mhe. George Simbachawene (katikati) kushoto ni Naibu Waziri wake Mhe. Ummy Nderiananga na  (kulia) ni  Kaimu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Bw. Raymond Kaseko na timu ya menejimenti wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya Michezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Licha michezo ikiwa ni ajira kwa wengine wanaoenda kwenye mashindano makubwa lakini kubwa ni kujenga afya mahusiano na kurelax kwakuwa huwezi kila siku uko ofisini tu unafanya kazi muda wote kwahivyo ni vizuri kuongeza ushiriki na wakati mwingine tutaweka ulazima wa watu kushiriki ilili tuibue vipaji vingine vilivyojificha.”alisema Waziri

Aidha Waziri Simbachawene amewataka viongozi wa Michezo wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wanaanzisha jogging club kwaajili ya kuendeleza michezo ili washiriki wanapokwenda SHIMIWI waweze kurudi na vikombe vingi zaidi.

“Hata ikiwezekana ofisi yote ya Waziri Mkuu ya Dodoma na Taasisi zake tuwe tunafanya Jogging angalau mara mbili kwa mwezi mimi na viongozi wengine tutakuwa mstari wa mbele tukiwa tumebeba bendera yetu ,tukifanya hivi kila mwezi visukari vitakimbia na michezo ya aina hiyo inatufurahisha na huu utaratibu ukiendelezwa hata tukishiriki SHIMIWI tunarudi na vikombe vingi”.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) Mhe.George Simbachawene (kulia) akikabidhiwa kikombe cha ushindi kutoka kwa mshindi wa kwanza katika Mchezo wa Drafti na Bw. Saidi Mwinshehe (kushoto) aliye shiriki  Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) iliyofanyika Mkoani Tanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Michezo Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Dotto Kyaolang amesema licha ya mpambano kuwa mkali wanamichezo wote walicheza kwa kiwango kilichotakiwa licha ya baadhi ya timu kutopata matokeo mazuri.

Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) ilifanyika Mkoani Tanga kuanzia tarehe 01 hadi 15, 2022 kwa kushirikisha wanamichezo kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu iliyoshirikisha wanamichezo 146, hivyo timu ya wanawake ya kuvuta kamba kuibuka kwa kupata ushindi wa Tatu na kwa upande wa Drafti kuibuka na ushindi wa Kwanza.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) Mhe. Ummy Nderiananga (aliyebeba kombe) kwenye picha ya pamoja na Timu ya wanawake ya mchezo wa kuvuta kamba kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!