WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi zitawasaidia wafanyabiashara kutathmini uwezo wao wa kibiashara au uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji.
“Wafanyabishara wakubwa kwa wadogo hutumia takwimu za sensa kutathmini uwezo wa kibiashara wa makampuni, uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji na kupitia takwimu za sensa, menejimenti na bodi za makampuni ya biashara na taasisi za uwekezaji za ndani na nje hupata uhakika wa kitakwimu ambao huwaongezea kujiamini na kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Agosti 15, 2022) wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi juu ya umuhimu wa ushiriki wao kwenye Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika nchini Agosti 23, 2022 kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo wanategemea takwimu za sensa kufanya maamuzi ya uwekezaji ikiwemo huduma mbalimbali kama maduka makubwa, upanuzi wa shughuli zao kama maghala ya kuhifadhia na kusambazia bidhaa, maeneo bora ya kutangaza biashara zao, masoko mapya na kubuni bidhaa mpya pamoja na aina ya huduma kama za hospitali, sehemu za starehe na sehemu za kufanyia mazoezi.
Amemshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia, kuthamini na kutilia mkazo mkubwa masuala ya takwimu na kuruhusu mwaka huu Tanzania ifanye Sensa kwa mujibu wa Miongozo ya Umoja wa Mataifa.
“Kitendo cha Mheshimiwa Rais kuridhia kutekeleza sensa ya sita mwaka huu kinaonesha uimara wa uongozi wa Kiongozi wetu na utekelezaji wa takwa hili ni kwa faida ya nchi yetu na ulimwengu kwa jumla.”
“Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu kwa kuwa moja ya mikakati ya kiuchumi ya Tanzania ni kuvutia uwekezaji na kuboresha kiwango cha maisha cha wananchi wake. Uwepo wa takwimu bora za Sensa ya Watu na Makazi utasaidia kuharakisha utekelezaji wa mikakati hiyo,” amesema Waziri Mkuu.
Akizungumzia umuhimu wa sensa kwa wafanyabiashara Waziri Mkuu amesema: “Kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara, sensa ni chanzo cha msingi cha taarifa za kidemografia na ukuaji wa soko la bidhaa na huduma katika nchi zote duniani. Takwimu zote za biashara zinahitaji takwimu za idadi ya watu kama kigezo cha msingi cha kufanya maamuzi ya uwekezaji, uzalishaji na biashara.”
Ametoa pongezi pia kwa vyombo vya habari kwa ushiriki wao mkubwa katika kutoa hamasa kwa jamii na kuwaelezea umuhimu wa sensa ikiwemo kuwajulisha kuwa sensa hiyo itafanyika lini. Amesema utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) Julai mwaka huu ulionesha kuwa asilimia 98 ya Watanzania wanatambua uwepo wa sensa