Home Kitaifa WAZIRI MKUU: SERIKALI IMEIMARISHA NGUVUKAZI SEKTA YA AFYA

WAZIRI MKUU: SERIKALI IMEIMARISHA NGUVUKAZI SEKTA YA AFYA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeimarisha nguvukazi kwenye sekta ya afya kwa kuongeza taasisi zinazotoa mafunzo ya afya na upatikanaji wa fursa za elimu ya juu kwa kada hiyo.

“Serikali imefanya upanuzi wa taasisi za mafunzo ya afya ili kuongeza idadi ya wahitimu. Taasisi hizo ni pamoja na vyuo vya uuguzi, ukunga na utabibu. Hivi sasa nchi yetu ina taasisi 182 zikiwemo taasisi 137 zinazomilikiwa na sekta binafsi. Ni jambo la faraja kuona kuwa katika mwaka 2023/2024 peke yake, vyuo hivyo vimedahili wanafunzi 40,000.”

Akizungumza na viongozi, wadau na watumishi walioshiriki ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kitaifa wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Afya leo (Jumanne, Julai 30, 2024), Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita imehakikisha fursa za masomo ya elimu ya juu zinapatikana kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa.

“Lakini pia, wanafunzi wanaosomea kozi za afya wamekuwa wakipewa kipaumbele wakati wote kwa kupewa mikopo ya asilimia 100. Vilevile, suala la kuendeleza rasilimali watu limeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kila mwaka ili kufanikisha ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi, stadi muhimu na wanaoweza kumudu mahitaji ya ndani na ushindani wa kimataifa,” amesema.

Akielezea kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali, Waziri Mkuu amesema Serikali imekwishaimarisha huduma ya afya ya msingi, huduma za afya katika ngazi ya wilaya na sasa inaimarisha huduma hizo kwenye ngazi ya Halmashauri.

“Tumeimarisha huduma za msingi, tumeimarisha hospitali za wilaya na sasa tunajenga hospitali za Halmashauri ili kupunguza umbali kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni. Sasa hivi tunaimarisha pia huduma za rufaa kama vile Benjamin Mkapa na Bugando,” amesema.

Akielezea kuhusu ajira na upangaji wa watumishi wa kada za afya, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, watumishi 30,000 wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi vikiwemo vya vijijini. “Baadhi ya watumishi hao ni pamoja na madaktari, wauguzi pamoja na wakunga. Hii ni hatua kubwa sana ya maendeleo katika utoaji wa huduma za afya nchini,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa upatikanaji wa rasilmaliwatu, vifaa tiba na dawa vinaendelea kuwa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo la siku mbili, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) imeandaa kongamano hilo kama sehemu ya kumkumbuka Hayati Rais Benjamin Mkapa lakini pia kutoa msisitizo wa haja ya kuendeleza rasilmaliwatu kwenye sekta ya afya.

Aliipongeza taasisi hiyo kwa kusimamia ndoto yao kuu ya kuzalisha watumishi kwenye sekta ya afya ambao kila wanapohitimu wamekuwa wanapangiwa ajira kwenye maeneo ya pembezoni kwa mkataba wa miaka mitatu. “Watumishi hawa wanafanya kazi nzuri sana huko waliko na wanapomaliza mkataba wao na taasisi hii, tumekuwa tunawachukua ili waendelee kutoa hudumakwa wananchi katika maeneo waliyoyazoea.”

Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Nassor Ahmed Mazrui alisema kwamba suala la uendelezaji wa rasilmaliwatu kwenye sekta ya afya ni la muhimu lakini akasisitiza haja ya kupigia debe utalii wa kitabibu (medical tourism) ili miundombinu inayoboreshwa iweze kuhudumia watu wanaokuja kutoka nje ya nchi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro alisema mkutano huo umehudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Akielezea mafanikio ya taasisi ya Benjamin Mkapa, Dkt. Senkoro alisema kupitia utoaji wa huduma za afya, wameweza kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 32 na wametoa ajira zaidi ya 13,000 kwenye sekta ya afya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!