Home Kitaifa WAZIRI MKUU: CHANGAMKIENI FURSA KUJENGA UCHUMI WA KIDIJITALI

WAZIRI MKUU: CHANGAMKIENI FURSA KUJENGA UCHUMI WA KIDIJITALI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanawake wote na Watanzania kwa ujumla waendelee kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na matumizi ya teknolojia katika kujenga uchumi wa kidijitali.

Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Machi 10, 2023) wakati akizungumza na wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Tano wa Mwanamke Kiongozi kwa mwaka 2023 uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliambatana na mahafali ya nane ya Programu ya Mwanamke Kiongozi ambapo jumla ya wahitimu 65 walitunukiwa vyeti. Washiriki 11 wa Programu hiyo walijidhamini wenyewe na wengine 54 wanatoka kwenye kampuni 29.

Akitoa msisitizo kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo, Waziri Mkuu amesema: “Wanawake wajitokeze kwa wingi kushiriki katika programu hii kwani imeendelea kuwa na matokeo chanya kwa washiriki na kuleta mabadiliko makubwa kwenye utendaji wao wa kazi na kugusa maisha yao binafsi.

Pia nitoe rai kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kiendelee kutoa mafunzo haya ya uongozi kwa wanawake pamoja na kuendelea kuwa vinara katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa maeneo ya kazi.”

Waziri Mkuu amesema suala la mabadiliko ya kidigitali ni moja ya vipaumbele vya Taifa kwani maendeleo ya uchumi yanategemea sana utandawazi. “Lakini pia katika mabadiliko haya ni muhimu kutambua mchango wa wanawake katika uchumi wetu na kutatua changamoto zinazowakabili wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya uchumi wa kidijitali.”

Amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa uchumi wa kidijitali, imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ambayo itaiwezesha nchi kutumia vema fursa za kiteknolojia zilizopo katika kuinua uchumi.

“Ili kutimiza azma hiyo, tayari Mkakati wa Taifa wa Brodibandi wa Mwaka 2021–2025 ambao utawezesha asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za intaneti yenye kasi ifikapo mwaka 2025 umeshaandaliwa. Serikali inaendelea na maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidigitali ili kuhakikisha nchi yetu haibaki nyuma katika ulimwengu wa kidijitali.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa mkutano huo, Waziri wa Nchi (OWM-Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako alisema ofisi yake kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wataendelea kusimamia sheria za kazi na masuala ya ajira nchini na kuweka mazingira rafiki katika sehemu za kazi.

Akielezea kuhusu suala la kima cha chini cha mshahara kwenye sekta binafsi, Prof. Ndalichako alisema: “Utekelezaji wa Kima cha Chini ulianza tarehe 1 Januari, 2023. Niwasihi ATE iendelee kutoa elimu na kuwasimamia wale ambao bado hawajatekeleza kikamilifu kwani hiyo ni haki ya kila mfanyakazi.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!