Home Kitaifa WAZIRI MKUU AZINDUA HUDUMA YA UPANDIKIZAJI ULOTO BENJAMIN MKAPA

WAZIRI MKUU AZINDUA HUDUMA YA UPANDIKIZAJI ULOTO BENJAMIN MKAPA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali iliamua kuwekeza shilingi bilioni 2.7 ili kuanzisha huduma ya upandikizaji uloto na kupunguza gharama za matibabu hayo kwa wananchi.

Kwa lugha nyingine, kuimarika kwa huduma za kibingwa na bobezi nchini kumepunguza gharama kubwa iliyokuwa inatumiwa na Serikali ili kuwezesha Watanzania wenye uhitaji kupata huduma hizo nje ya nchi. Kwa mfano, huduma hii ya upandikizaji uloto ikitolewa katika hospitali hii, itagharimu shilingi milioni 50 hadi 55 kwa mgonjwa mmoja,” amesema.

Amesema hayo leo (Jumatano, Mei 10, 2023) wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma mara baada ya kuzindua huduma za kibingwa za upandikizaji wa uloto (Bone Marrow Transplant) hasa kwa watu wenye Seli Mundu (Sickle Cell).

Waziri Mkuu amesema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa inakuwa hospitali ya pili baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuzindua huduma hiyo ya upandikizaji wa uloto na hivyo, kuifanya kuwa miongoni mwa hospitali chache zinazotoa huduma hiyo katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Upandikizaji uloto unatoa nafuu kubwa sana kwa wagonjwa wa seli mundo kwani huwapunguzia kwa kiasi kikubwa maumivu na maambukizi ya mara kwa mara na wakati mwingine huwa sababu ya kupona kabisa kwa ugonjwa huu wa kudumu. Kutokana na nafuu hiyo, mgonjwa huweza kuishi maisha yenye ubora na kushiriki vema katika shughuli mbalimbali ikiwemo masomo”.

Amesema uzinduzi wa huduma hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ni ushahidi tosha wa namna ambavyo Tanzania inapiga hatua kuboresha huduma za afya. “Huduma za namna hii kuendelea kutolewa katika hospitali zetu si jambo dogo, na hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa huduma kama hizi zinapatikana katika nchi chache sana kwenye bara la Afrika.

Nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa rasilimali fedha kwa ajili ya kununulia vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na dawa pamoja na kuwaendeleza kielimu wataalamu wetu katika ngazi za ubingwa na bobezi,” amesema.

Kabla ya kuzungumza na hadhira hiyo, Waziri Mkuu alitembelea wodi za kitengo maalum cha upandikizaji uloto na kuzungumza na watoto na wazazi wenye watoto waliopatiwa tiba hiyo. Wote waliishukuru Serikali kwa kuanzisha huduma hiyo kwani imewasaidia watoto wao kuondokana na maumivu ya mara kwa mara na kutumia muda mwingi kwenda kliniki ya seli mundu kupata matibabu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!