WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa Majaliwa amewasili leo Januari 18, 2024 nchini Uganda akimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali zisizofungamana na Upande wowote (NAM) ulioanza tarehe 15 – 20 Januari, 2024.
Pia, Mheshimiwa atamwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia katika mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la G77+China utakaofanyika tarehe 21-22 Januari, 2024, Kampala – Uganda.
Ujumbe wa Waziri Mkuu katika Mikutano hiyo utajumuisha viongozi waandamizi wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa January Makamba.
Mkutano wa NAM hufanyika kila baada ya miaka mitatu na Mkutano wa mwisho, wa 18 ulifanyika jijini Baku nchini Azerbaljan mwezi Oktoba, 2019. NAM ni umoja wa nchi na Serikali 120 zenye msimamo wa sera ya kutofungamana na upande wowote.