Home Kitaifa WAZIRI MKUU AISHUKURU SERIKALI YA DENMARK, AAGANA NA BALOZI WAKE

WAZIRI MKUU AISHUKURU SERIKALI YA DENMARK, AAGANA NA BALOZI WAKE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya Denmark kwa misaada ambayo imekuwa ikiitoa kwenye miradi ya maendeleo nchini ambapo Krona milioni 1.95 (sh. bilioni 645.86) zilizotolewa katika kipindi cha miaka mitano.

Ametoa shukrani hizo leo (Jumatatu, Julai 15, 2024) wakati akizungumza na Balozi wa Denmark anayemaliza muda wake nchini, Bi. Mette N. Dissing-Spandet kwenye ofisi ndogo ya Magogoni, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Serikali hiyo ilisaidia sana kwenye miradi mbalimbali hasa katika sekta za afya, masuala ya kikodi, shughuli za utafiti, hifadhi ya mazingira na kuimarisha demokrasia na utawala bora.

“Ninakushukuru kwa jitihada zako katika kipindi chote cha miaka mitano uliyokuwepo hapa nchini kwani umesaidia kuimarisha mahusiano yaliyokuwepo baina ya nchi hizi mbili tangu miaka ya 60. Pia tumenufaika na programu za kubadilishana wataalamu baina ya nchi zetu,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema kutokana na changamoto za kiuchumi zilizokuwepo duniani, mwaka 2020 nchi hiyo ilitaka kupunguza idadi ya balozi zake barani Afrika, Tanzania ikiwemo. “Lakini Serikali yetu ilimtumia Balozi huyu kuelezea haja ya kuendelea na mahusiano baina ya nchi zetu mbili na ikafanikiwa, ndiyo maana tunatarajia kumpokea balozi mwingine hivi karibuni.”

Waziri Mkuu amesema anatarajia kuwa Balozi ajaye ataendeleza mazuri ya mtangulizi wake ikiwemo kukamilisha mpango wa kuandaa kongamano la wafanyabiashara baina ya Tanzania na Denmark ili kuwaalika wawekezaji kwenye sekta za nishati, kilimo biashara na viwanda.

Amemuomba Balozi huyo akisharejea kwao, aendelee kuwa Balozi mzuri wa kuitangaza Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ambayo ameyaona hapa nchini.

Kwa upande wake, Balozi Dissing-Spandet alimweleza Waziri Mkuu anaondoka nchini akiwa anaacha mahusiano baina ya nchi hizo mbili yakiwa kwenye mikono salama kwa sababu Balozi anayekuja kuchukua nafasi yake ni mwanadiplomasia mzoefu.

“Ninaondoka nchini nikiwa na furaha kwa sababu mahusiano ya Tanzania na Denmark yamerudi kwenye hali yake ya awali. Ninashukuru kwa kipindi chote cha miaka mitano nilichoishi hapa nchini, mbali na changamoto za UVIKO-19 na za kiuchumi duniani, kilikuwa ni kizuri sana na hakitasahaulika maishani mwangu,” alisema Balozi huyo.

Amesema anaamini kuwa Balozi mpya ajaye atasimamia suala la uwekezaji ikizingatiwa kwamba nchi hiyo inaandaa mkakati mpya wa kuboresha mahusiano baina yake na nchi za Kiafrika, hasa kwenye eneo la uwekezaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!