Na Mathias Canal, Rombo
Mbunge wa Jimbo la Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda tarehe 20 Julai 2022 ametembelea na kuwasalimu wagonjwa katika hospitali ya Wilaya ya Rombo-Huruma ambayo ipo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Moshi akiwa katika siku ya pili ya ziara yake jimboni humo.
Prof Mkenda amesema kuwa serikali itaendelea kufuatilia upatikanaji wa majukumu yote ya msingi ikiwemo upatikanaji wa madaktari bingwa pamoja na upatikanaji wa kutosha wa vifaa tiba.
Amesema kuwa huduma zinazotolewa na taasisi za dini ni wazi kuwa zinatolewa kwa lengo kuu la kuhudumia wananchi lakini sio kwa ajili ya faida kama ilivyo katika taasisi zingine.
Amesema kuwa hospitali hiyo kama alivyosisitiza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Philip Isdor Mpango wakati akiweka jiwe la msingi ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Rombo, ambapo alisema kuwa ukubwa wa Wilaya ya Rombo unatakiwa kuwa na hospitali mbili za wilaya.
Mhe Mkenda amewapongeza madaktari, wauguzi na uongozi wa Hospitali hiyo kwa ujumla kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya kuhakikisha wanaokoa maisha ya wananchi hususani wakazi wa Rombo.
Ameahidi kufuatilia na kutatua changamoto ya upungufu wa watoa huduma ya afya katika hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya kadhia ya barabara inayoenda hospitalini hapo.
Kuhusu changamoto ya maji, Mbunge huyo amesema kuwa changamoto hiyo itapatiwa ufumbuzi hivi karibuni kwani tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni 10 kwa ajili ya miradi ya maji wilayani Rombo
MWISHO