Na Mathias Canal, Dodoma
Katika Bajeti iliyopitishwa Bungeni Jijini Dodoma ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2022/2023 serikali imetenga jumla ya Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya Ufundi stadi (VETA) katika Wilaya 62 nchini.
Kufuatia kupitishwa kwa bajeti hiyo serikali imeitaka VETA kukamilisha haraka michakato ya ndani na kuanza ujenzi wa vyuo hivyo mwezi Januari mwaka 2023.
Akizungumza leo tarehe 21 Disemba 2022 Jijini dar es salaam wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara na VETA, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) ameutaka uongozi wa VETA kuhakikisha ujenzi huo unaanza mwishoni mwa mwezi Januari 2023 na mipango iwe madhubuti.
“Muanze ujenzi kwa mipango madhubuti ili watu waliopo nje wakiangalia waone kweli hii ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na taasisi zake zinafanya kazi inayotakiwa” Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa uongozi wa VETA kwa asilimia kubwa una makaimu watendaji wengi hivyo mafanikio ya kazi hiyo pekee yatatoa fursa ya viongozi hao kupewa nafasi kubwa zaidi kwa kushikilia nafasi hizo na sio kukaimu.
“Mapendekezo yapo mezani kwangu ya nani awe mtendaji na huu mchakato utanipa mwanga vizuri wa nani awe mtendaji, tangu tupitishe Bajeti mpaka sasa hivi hakuna hata jembe limeanza kuchimba msingi kidogo tumechelewa” Amesema Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa VETA inafundisha elimu ya ufundi hivyo kupewa jukumu la ujenzi ni kutaka ionyeshe kwa vitendo ni kwa kiasi gani inafundisha taaluma inayoiweza.
MWISHO