Asema imefikisha asilimia 37
Kiasi cha Shilingi bilioni 41.6 kinatarajiwa kutumika katika kulipa fidia mgodi wa kabanga Nikeli
Kutokana na Mabadiliko ya Sheria ya Mwaka 2017 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeongeza umiliki wa hisa katika Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Almasi ijulikanayo kama Williamson Diamonds Limited na kufikia asilimia 37 tofauti na awali ilikuwa na asilimia 25.
Kupitia mabadiliko hayo Serikali imeweza kusaini mikataba ya ubia na kuunda kampuni tano za ubia kwa ajili ya uchimbaji madini Wa kati na uchimbaji mkubwa , kampuni hizo ni pamoja na Tembo Nickel Corporation Ltd, Sotta Mining Corporation Ltd, Faru Graphite Corporation Ltd, Duma TanzGraphite Ltd na Mamba Minerals Corporation Ltd.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu uendelezaji wa leseni za madini , Mhe.Waziri Mavunde alisema kuwa tarehe 19 Januari 2021 Serikali kupitia kampuni ya Tembo Nikeli (TNCL) iliingia ubia wa umiliki wa asilimia 16 na Kampuni ya LZ Nickel ya Uingereza yenye hisa asilimia 84 kwa mradi wa uchimbaji madini ya Nikeli katika mkoa wa Kagera wilayani Ngara.
Akielezea maendeleo ya mradi huo Mhe.Mavunde alieleza kuwa uzalishaji wa mbale ya Nikeli pamoja na madini ambata unatarajiwa kuanza mwaka 2026 baada ya kukamilisha hatua za ulipaji wa fidia kwa wananchi na kuanza usimikaji wa mitambo.
Aidha, aliongeza kuwa mpaka kufikia mwezi Oktoba 2023 , kampuni ya TNCL ilikuwa imekamilisha uthaminishaji wa wananchi 1,341 na kuweza kulipa kiasi cha Shilingi za kitanzani bilioni 33.08 kama fidia kwa wananchi wakaopisha mradi katika vijiji vya Bugarama, Rwinyana, Nyabihanga , Mukubu, Mumiramira na Muganza ambapo mpaka kukamilika kiasi cha Shilingi bilioni 41.6 za kitanzania zinatarajiwa kutumika.
Mradi wa uchimbaji madini ya Nikeli una maeneo mawili ambapo eneo la kwanza lina hekta zaidi ya 4,000 zimetengwa kwa ajili ya uchimbaji mkubwa wa madini ya Nikeli wilayani Ngara eneo la Kabanga, ambapo uchimbaji mkubwa utafanyika kwa kipindi cha miaka 33 na eneo la pili ni kiwanda cha kusafishia madini kinachojengwa katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, mradi huu unatarajia kutoa fursa za ajira 978.
VISION2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI