Home Biashara WAZIRI MAVUNDE ATINGA SOKO LA DHAHABU KAHAMA USIKU,DHAHABU KILO 4 YAKAMATWA IKITOROSHWA.

WAZIRI MAVUNDE ATINGA SOKO LA DHAHABU KAHAMA USIKU,DHAHABU KILO 4 YAKAMATWA IKITOROSHWA.

Katika kuhakikisha inalinda rasilimali madini ili ziweze kuchangia maendeleo ya Nchi na kuinua uchumi wa watanzania, Serikali imesimamisha leseni zote Nchi nzima za Kampuni ya Nadoyoo Mineral Trading kufuatia kukamatwa kwa mmoja wa wahusika wa Kampuni hiyo akitorosha dhahabu takribani kilo 4.3 zenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 562,288,207.

Hayo yamesemwa jana tarehe 11 Oktoba, 2023 usiku na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Wilayani Kahama baada ya kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan haitakubali kuona watu wachache wanajihusisha na vitendo hivi viovu vya kutorosha madini. Nataka niwaambie, tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote tutakayemkamata akijihusisha na utoroshaji wa madini”

“Ninapoingia Wizara ya Madini mwezi mmoja uliopita nilisema, ukitaka kufahamu sura yangu nyingine basi jaribu kutorosha madini. Sasa basi, kuanzia leo mtu yeyote atayekamatwa kwa kosa la kutorosha madini, tutakwenda kusimamisha leseni zake zote Nchi nzima wakati tukisubiri hukumu ya vuombo vya sheria, na iwapo mahakama itabaini mhusika ana hatia, tutakwenda kuchukua hatua kali ikiwemo kufuta kabisa leseni zote na kuhakikisha hatajihusisha tena na biashara ya madini nchini” aliongeza Mhe. Mavunde.

Sambamba na hilo, Mhe. Mavunde alitoa wito kwa wafanyabiashara wa madini kuwa wazalendo kwa kufuata taratibu zilizopo na kulipa tozo, ada na kodi mbalimbali ili kuiwezesha Serikali kupata mapato na kuendelea kuimarisha huduma kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara, umeme, afya na elimu.

Pia, Mheshimiwa Mavunde alionesha utayari wa kutenga siku na kukaa pamoja na wafanyabiashara wa madini ili kwa pamoja wamweleze hasa ni nini wanadhani inaweza kuwa ni changamoto kubwa inayopelekea baadhi yao kufikia hatua ya kujihusisha na vitendo vya utoroshaji madini, hatua ambayo anaamini itasaidia Serikali kuchukua njia sahihi kushughulikia suala hilo.

Vilevile, Mheshimiwa Mavunde alieleza bayana kuwa pamoja na hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watoroshaji wa madini, pia madini yote yatakayokamatwa yatahifadhiwa na Serikali na kupelekwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kusubiri hatma ya Mahakama.

Awali, akieleza taarifa ya masoko ya dhahabu, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Madini Kahama, Bw. Jeremiah Hango alibainisha kuwa takribani kilo 562.3 za dhahabu zenye thamani ya shilingi bilioni 74.8 ziliuzwa katika masoko na vituo vya madini kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01 Julai, 2023 hadi 10 Oktoba, 2023.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mheshimiwa Mboni Mhita alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini na kuahidi kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha vitendo vyote vya utoroshaji wa madini vinakomeshwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!