Na Magrethy Katengu
Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya Watu Dkt Angelina Mabula amesema Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ameridhia ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,492,703 iliyokuwa sehemu maeneo ya Umma ikiwemo hifadhi za Utalii Ranchi za Serikali kumegwa na kurasimishwa kwa wananchi.
Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari kuzungumzia masuala mbalimbali ya sekta ya ardhi na muelekeo wa utekezaji wa Wizara hiyo kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2022 uliofanyika jijini Dar es Salaam amesema Mapori Tengefu 12 yenye ukubwa ekari 707,962 na Hifadhi za Misitu Misitu 7 zenye ekari 46,715 nayo imefutwa na ardhi hiyo kukabidhiwa kwa wananchi kupitia usimamizi wa Serikali za Mikoa katika kupanga na kuyapima maeneo hayo hivyo sekta ya hiyo ni muelekeo wa utekezaji wa Wizara hiyo kwa kipindi cha kuanzia Januari 2023.
“Naielekeza Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Mikoa kusimamia utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kwenye maeneo yao yote yalioainishwa na kutolewa uamuzi na mongoni mwa kazi za kutekelezwa hivi sasa ni pamoja na uwekaji wa alama za mipaka baina ya maeneo ya hifadhi na maeneo ambayo Serikali imeridhia yabaki kwa wananchi, upangaji na upimaji wa maeneo yaliyorejeshwa kwa wananchi, utambuzi, uhakiki na uthamini wa maeneo ambayo wananchi watatakiwa kupisha shughuli au maeneo yatakayotumika kwa matumizi ya umma na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi” amesema Dkt. Mabula
Amechukua fursa kupitia mkutano na vyombo vya habari kuomba kila Mkoa kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Serikali na kuhakikisha kazi zote zinakamilishwa ifikapo tarehe 30 Machi, 2023.
Dkt. Angelina Mabula amefafanua ulipaji kodi ya pango la ardhi hasa baada ya msamaha wa riba ya malimbikizo ya pango la ardhi uliotolewa na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo wananchi wenye malimbikizo walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili wasamehewe riba ya malimbikizo. hivyo ameleza kuwa, Kutokana na nafuu uliotolewa Wizara yake imeweza kukusanya jumla ya Tsh 90,907,939,421 sawa na asilimia 75 ya lengo la nusu mwaka.
Sanjari na hayo amesema hadi kufikia Novemba, 2022 wananchi 2,819 wamenufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi yenye jumla ya TZS 6,946,930,272. Idadi hiyo haijumuishi wananchi waliojitokeza ambao wamehudumiwa kuanzia tarehe 1 – 31 hadi Disemba 31, 2022.
Pia amewashukuru na kuwapongeza wamiliki wa ardhi waliojitokeza kunufaika na msamaha uliotolewa na Mhe. Rais na kubainisha kuwa, katika mwezi Disemba, 2022 Wizara ya Ardhi imeshuhudia idadi kubwa ya wamiliki waliojitokeza kulipa na kiasi cha bilioni 22.6 kimekusanywa katika mwezi Disemba pekee.
Waziri Mabula Akigeukia suala la utatuzi wa migogoro ya ardhi, Dkt Mabula amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu mipango ya jumla, mipango kina na mipango ya matumizi ya ardhi vijijini kupitia kamati za ardhi za Vijiji ili kudhibiti ujenzi holela usiozingatia mipango iliyoandaliwa na kuidhinishwa kupitia Kamati za Mipangomiji.
“Wizara imekuwa ikipokea taarifa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukiukwaji wa taratibu mbalimbali zinazohusu Usimamizi wa Ardhi Mijini na Vijijinina miongoni mwa malalamiko ni baadhi viongozi wa vijiji na Mitaa kuuza ardhi kinyume na utaratibu, kukosekana kwa udhibiti wa uendelezaji ardhi katika maeneo ya Vijiji na Miji. Hali hiyo imesabisha kuongezeka kwa migogoro ya ardhi na uendelezaji ardhi kinyume na mipango iliyoandaliwa na kuidhinishwa” amesema Waziri
Dkt Mabula amesema Wizara yake inaandaa programu maalum ya kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa Mamlaka za Upangaji taarifa hizi zitatolewa kwa umma kama sehemu ya uwajibikaji wa mamlaka zetu kwa wananchi.
Kuhusu ujenzi wa vituo vya mafuta, Dkt Mabuka amesema hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2022 Wizara imepokea taarifa ya uendelezaji wa vituo vya mafuta kutoka Halmashauri 129 kati ya 184 zilizopo nchini sawa na asilimia 70.1.
Uchambuzi uliofanywa na Wizara ya Ardhi umebaini katika Halmashauri 129, kuna vituo 2,063 ambapo kati ya hivyo vituo vya mafuta ni 1269 (asilimia 61.6) na vituo vidogo vya mafuta ni 794 (asimilia 38.5) huku Vituo 1,868 vimejengwa katika umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka kituo kimoja na kingine sawa na asilimia 90.5 kama inavyoelekezwa na kanuni ya viwango vya umbali
Hata hivyo , Vituo 195 vimejengwa umbali wa chini ya mita 200 sawa na asilimia 9.5. Wizara inaendelea kufanya uchambuzi zaidi ili kubainisha vituo ambavyo vimejengwa kabla au baada ya kanuni za mwaka 2018 zinazoendelea kutumika ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.
Pia Waziri wa Ardhi amezungumzia suala la program ya miaka 10 ya urasimishaji makazi holela ambapo Wizara inayo Programu ya Urasimishaji Makazi iliyoanza kutekelezwa mwaka 2013. Programu hiyo mwisho wake ni mwaka huu 2023 na imekuwa ikitekelezwa katika Mitaa 3,397 kwenye Mikoa yote 26.
Dkt Mabula amesema, Mitaa 1,961 imerasimishwa sawa na asilimia 57.7 na Mitaa 1,436 haijarasimishwa sawa na asilimia 42.3 na kubainisha kuwa prrogramu hiyo imewezesha upangaji wa viwanja 2,338,926 na kati ya hivyo, viwanja 1,170,638 upimaji wake umekamilika. Aidha, jumla ya milki 177,330 zimeandaliwa na kutolewa kwa wananchi.
Hata hivyo, amesema katika kutekeleza Programu hiyo, kumekuwepo na changamoto mbalimbali licha ya mafanikio yaliyopatikana na kuzitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na Uelewa mdogo wa wananchi juu ya umuhimu na namna zoezi la urasimishaji linavyofanyika, baadhi ya wananchi kutokuwa tayari kuchangia ardhi inayohitajika kwa ajili ya miundombinu na matumizi ya umma, baadhi ya wananchi kutolipa gharama za urasimishaji kwa wakati hali inayosababisha baadhi ya kampuni kushindwa kumudu gharama za utekelezaji na baadhi ya kampuni za urasimishaji kutokamilisha kazi kwa wakati pamoja na kutumia wataalam wasiokuwa na sifa.
Hata hivyo, amesema kutokana na uwepo wa changamoto hizo, Wizara imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kazi za urasimishaji zinakamilika na hatua hizo ni pamoja na Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri, kukwamua baadhi ya kazi zilizokwama, kuchukua hatua kwa kampuni zilizoshindwa kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kusimamisha au kufungia baadhi ya kampuni hizo, kuhusisha taasisi za kifedha katika miradi ya urasimishaji na kuandaa na kusambaza mwongozo wa urasimishaji ikiwemo kupunguza gharama za urasimishaji hadi kufikia shilingi 130,000 kwa kiwanja.
Pamoja na jitihada hizo, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri na Sekta Binafsi inatekeleza programu ya Kupanga, Kupima na kumilikisha ardhi ili kuwa na miji nadhifu na iliyopangwa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Matokeo ya programu hii, yatasaidia kupunguza Mitaa isiyorasimishwa na kudhibiti kuendelea kukua kwa makazi yasiyopangwa. Aidha, baadhi ya Mitaa ambayo haijarasimishwa (Mitaa 559) imeingizwa kwenye Mradi wa Kuboreshaji Milki za Ardhi (Land Tenure Improvement Project) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo utekelezaji wake umeanza.
Wizara imeandaa Mkakati wa kushughulikia changamoto za urasimishaji baada ya kikao baina ya Wataalam wa Wizara na wadau wa urasimishaji kilichofanyika tarehe 22 Disemba, 2022. Mkakati huo, utawasilishwa kwenye kikao nilichopanga kukiongoza mapema wiki ijayo hapa Dar es Salaam ambapo ndiyo penye changamoto kubwa ya zoezi la urasimishaji.