Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula, ameipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kubuni mfumo wa NAPA (National Physical Addressing System) ambao umewezesha kupatikana kwa taarifa zinazotumika katika kurahisisha uhuishaji wa kumbukumbu za wamiliki wa ardhi.
Waziri Mabula ametoa pongezi hizo leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24.
Waziri Mabula alisema kuwa, katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa taarifa sahihi za wamiliki wa ardhi, Wizara inaendelea kuhuisha kumbukumbu na kuziingiza katika Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa urahisi, usahihi na kwa muda mfupi ambapo uhuishaji
huo unahusisha uhakiki wa taarifa za namba za simu za wamiliki, uoanishaji wa namba za NIDA, ukubwa wa viwanja, matumizi na mahali vilipo.
“Uhakiki huu unafanyika kwa kutumia taarifa zilizokusanywa katika zoezi la Anuani za Makazi na Sensa ya Watu na Makazi pamoja na kumbukumbu za viwanja husika. Aidha, naishukuru Wizara ya Habari kwa mradi wa NAPA kwa kuwa mfumo huu utasaidia ukusanyaji na ufuatiliaji wa kodi ya pango la ardhi kwa kutumia majira ya nukta na usimamizi wa uendelezaji wa miji”, alieleza Waziri Mabula.
Waziri Mabula amefafanua kuwa, hadi Mei 15, 2023 Wizara yake imehuisha kumbukumbu za wamiliki wa ardhi 635,833 kati ya 500,000 zilizopangwa kuhuishwa kufikia Juni 2023 ambayo ni sawa na asilimia 127 ya lengo ambapo zoezi hilo linatekelezwa kwa kutumia wataalam kutoka Serikalini na wataalam wa muda.
“Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza kwa kazi kubwa na ya kizalendo ambayo imewezesha uchakataji kidigitali wa taarifa hizo ambapo katika mwaka 2023/24, Wizara itaendelea na zoezi la kuhuisha kumbukumbu za ardhi”, alisema Waziri Mabula.