Home Kitaifa WAZIRI KAIRUKI AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA NA KUTOA ELIMU KWA JAMII ILI...

WAZIRI KAIRUKI AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA NA KUTOA ELIMU KWA JAMII ILI KUWEZESHA UHIFADHI ENDELEVU

Na Mwandishi wa NCAA, Babati Manyara.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa mwelekeo wa serikali kwa sasa ni kujikita katika matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na misitu ili kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelevu kwa vizazi vya sasa na baadae.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani yaliyofanyika leo tarehe 3 machi, 2024 Babati Mkoani Manyara.

“Pamoja na matumizi ya teknolojia kwenye uhifadhi, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuongeza ulinzi kwa wanyamapori ili kupambana na ujangili wa nyara na Kupunguza migongano kati ya wanyamapori na wananchi na kuhakikisha kuwa wanyama wanakuwa salama kwenye Hifadhi zetu” Alisema Kairuki.

Aidha, Waziri Kairuki amezitaka taasisi za uhifadhi kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii ili iweze kuwa sehemu ya uhifadhi endelevu na kupunguza vitendo vya ujangili wa rasilimali za wanyamapori na misitu.

Akiongea katika maadhimisho hayo mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Fortunata Msofe alisema shughuli za ulinzi wa wanyamapori na misitu ni la kufa na kupona kwa wadau wote wa uhifadhi ndio maana katika maadhimisho ya nwaka huu wamekuja na kauli ya kuwa kauli mbiu isemayo “Kuunganisha watu na ulimwengu, kuvumbua matumizi ya teknolojia ya kisasa kuhusiana na uhifadhi wa wanyamaopori” .

Dkt. Msofe amebainisha kuwa uamuzi wa kutumia teknolojia katika uhifadhi unalenga kutatua changamoto za migongano ya binadamu na wanyamapori.

Akiongea kwa niaba ya Kamishina wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Afisa Uhifadhi Mkuu wa NCAA Dismas Macha amesema NCAA kwa sasa inatumia njia mbalimbali za kiteknolojia ili kuhakikisha wanyamapori wanabaki salama kwenye mazingira yao bila kuathiri shughuli za kibinadamu

“Tunatumia njia mbalimbali kama visikuma mawimbi, mifumo ya GPS, kamera za kufuatilia mienendo ya wanyama, ndege zisizo na rubani “drones” na nyinginezo ambazo zinazotumia teknolojia ya kisasa kutuwezesha kuimarisha ulinzi na usalama wa wanyamapori ndani ya Hifadhi.

Amebainisha kuwa njia hizo zinasaidia kukusanya taarifa za Wanyama pale wanapotoka au kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine hasa wale Wanyama hatarishi wanaotoka hifadhini na kuingia kwenye makazi ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi” alisema Macha.

Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) ni miongoni mwa taasisi za Wizara ya Maliasili na utalii zinazoshiriki maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani 2024 yanayofanyika kitaifa Wilayani Babati Mkoa wa Manyara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!