Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Plan International Dkt. Mona Girgis ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma leo Oktoba 26, 2022.
Katika mazungumzo yao Dkt. Mona na aliyeambatana na Ujumbe wake aliwasilisha programu ya utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo hapa nchini yakiwemo ulinzi wa mtoto, maji na usafi wa mazingira.
Pia alimuelezea Waziri namna Plan International inavyoshiriki katika jitihada za mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi zinazokumba Tanzania na dunia kwa ujumla.
Alisema shirika hilo linatarajia kushiriki katika Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika nchini Misri Novemba 2022.
Waziri Jafo alipongeza jitihada za shirika hilo za kuunga mkono Serikali katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema Serikali itakuwa bega kwa bega na washirika wa maendeleo wakiwemo Plan International ili kuimiza malengo ya kuhakikisha hali ya uhifadhi wa mazingira inaimarika.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi Dkt. Andrew Komba, Mtaalamu wa Mawasiliano na Uchechemuzi Bi. Cesilia Bosco na Mtalaamu wa masuala ya Uchechemuzi Zuhura Mbura kutoka Shirika la Plan International.