Home Kitaifa WAZIRI JAFO AAGIZA UCHUNGUZI WA BIASHARA ZINAZOENDESHWA KINYUME CHA SHERIA

WAZIRI JAFO AAGIZA UCHUNGUZI WA BIASHARA ZINAZOENDESHWA KINYUME CHA SHERIA

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt. Selemani Jafo (Mb) ameagiza kufanyika kwa tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya Ripoti ya mazingira ya biashara baina ya wazawa na wageni nchini kwa kila baada ya miezi sita.

Katika kufanikisha hilo amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuunda timu maalum na kuweka mpango kazi wa kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mapendekezo hayo.

Amebainisha hayo wakati akipokea ripoti hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati Prof. Edda Tandi Lwoga ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Machi 17,2025 jijini Dar es salaam.

Dkt. Jafo amesema kuwa kwa munibu wa kamati hiyo taarifa zilizokuwa zikitolewa kuhusu changamoto za biashara nchini zimethibitishwa kuwa za kweli.

Aidha Dkt. Jafo ameagiza Idara ya Kazi na Uhamiaji kuanza mara moja msako katika maeneo ya Kariakoo ili kubaini watu wanaofanya kazi na biashara kinyume na taratibu za nchi na kusisitiza kuwa operesheni hiyo isihusishe Kariakoo pekee bali iendelee hadi mikoani.

Pamoja na hilo pia Dkt.Jafo ameziagiza Taasisi ya Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Ushindani (FCC) kufanya operesheni maalum ya kufuatilia malalamiko kuhusu uwepo wa bidhaa zisizo na ubora ambazo zinaathiri biashara na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.

Vilevile Dkt. Jafo amesema kuwa Kwa mujibu wa ripoti hiyo, imebainika kuwa baadhi ya biashara zinaonekana kumilikiwa na wageni, kwa mujibu wa nyaraka, zimesajiliwa kwa majina ya wenyeji wa Tanzania hivyo inapelekea changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wa Kitanzania huku vijana wakitumika kuhujumu nchi yao kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wasiofuata sheria.

Pia, ameeleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao bila kusajiliwa na Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) au Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), jambo ambalo linaathiri biashara halali nchini.

Waziri Jafo ameongeza kuwa ripoti hiyo imebaini vikwazo mbalimbali vilivyokuwa vikikwamisha kazi ya kamati kwa kuzuia kamati kufanikisha majukumu yake. Hata hivyo, amesema ripoti hiyo imewezesha kufichua changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya biashara hivyo itawasilishwa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!