Na Mwandishi wetu, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima amewataka maofisa Ustawi wa Jamii kufanya utambuzi wa watoto katika maeneo yao ili kuzuia watu wanaowatumia kwa shughuli zisizofaa.
Akizungumza katika mkutano wa wanataaluma, wataalam na wadau wa Ustawi wa Jamii Dk. Gwajima amesema kama kila mmoja atasimamia wajibu wake pale alipo hakutakuwa na suala la Watoto waliopo katika mazingira yasiyokuwa rasmi ambao wamejiingiza katika kuomba mitaani.
Amewaagiza Maofisa hao kuwa na daftari maalum la watoto ambalo litaainisha changamoto za kila mmoja na wale wenye mahitaji maalum na wasiokuwa wasiokuwa na makazi wapelekwe kwenye makazi maalum.
Dk. Gwajima amesema uwepo wa watoto wanaoomba mitaani unawanufaisha watu wachache ambao wanaowatumia watoto hao na kuzinufaisha familia zao.
“Hawa watoto utakuta kwa siku anapata Sh. 10,000 au 15,000 mara miaka mitatu ni shilingi ngapi? na unaweza kujiuliza wanaweka kwenye benki gani kama siyo kutumika kama miradi ya watu” Dk. Gwajima
Katika hatua nyingine Waziri Gwajima amesema vipo vituo 30 vya malezi vilivyojengwa na wadau ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa jamii na kueleza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha zaidi ili kujenga vituo zaidi.
Aidha Waziri Gwajima amesema maofisa Ustawi wa Jamii ni madaktari wa Jamii na wanahitajika katika kila eneo lenye ikiwemo kwenye nyumba za Ibada.
Amesema hata katika masuala ya afya ya akili ambayo yametajwa kuongezeka katika siku za karibuni maofisa Ustawi pia wanahusika katika kutoa unasihi na kupunguza changamoto hiyo ambayo amewataka kutafuta chanzo cha ongezeko lake.
Waziri Gwajima amesema kutokana na kuwepo kwa uhusiano baina ya afya ya akili na matumizi ya Dawa za kulevya maofisa hao wanapaswa pia kushiriki katika vita ya dawa za kulevya.
Kuhusu kuwepo kwa ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia amesema wakati wa kutokomeza vitendo hivyo umefika kwa kutoa elimu na kufanya kazi karibu na jamii ili wanajamii wafunguke wanapokutana na changamoto.
Kuhusu sheria ya Ustawi Waziri Gwajima amesema sheria hiyo ni ya muhimu maana itafanya utambuzi wa wana taaluma ya Ustawi na kutoa Ithibati na leseni kwa wanataaluma hao.
Mwisho