Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki ambaye kwa sasa ameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mshauri wa Rais.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Mtumba jijini Dodoma ambapo Mhe. Chana ameshukuru kwa kukabidhiwa vitendea kazi muhimu vitakavyosaidia katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Nitoe shukrani kwa kupata vitendea kazi hivi na nikuahidi ushirikiano na niseme milango iko wazi. Tunajua kuna maeneo mengi sana utaendelea kutushauri” Mhe. Chana amesisitiza.
Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Angellah Kairuki pamoja na wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi kwa mafanikio yaliyopatikana.
Aidha, ameendelea kumshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu kwa imani kubwa ambayo amewapatia na kwa uongozi wake mahiri na makini na kuahidi kuhakikisha kuitendea haki imani hiyo.
Kwa upande wake, Mhe. Kairuki amewashukuru watumishi na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa namna ambavyo wamefanya kazi na kuwezesha mafanikio yaliyopatikana.
“Tumeweza kulinda hifadhi na Rasilimali za Taifa, kuendeleza miradi ya ufugaji nyuki, utunzaji misitu, uhifadhi wa faru na mingine, kuhimiza utalii rafiki na endelevu kwa mazingira ili kuvutia na kuchochea utalii.” Mhe. Kairuki amefafanua.
Ameongeza kuwa katika kipindi chake, mafanikio mengine yaliyopatikana ni ongezeko la idadi ya Watalii hadi kufikia zaidi ya milioni 1.9, kukuza na kuzindua miradi mingi ya utalii,uwekezaji katika huduma za malazi, kutumia wanyamapori kuwa kichocheo kikubwa cha kuhifadhi mazingira na kuongeza uelewa wa umuhimu wa utalii hasa utalii wa ndani.