Home Kitaifa WAZIRI AWESO: WATAKWIMU NA WATEHAMA WAWEZESHWE KUKUSANYA TAKWIMU

WAZIRI AWESO: WATAKWIMU NA WATEHAMA WAWEZESHWE KUKUSANYA TAKWIMU

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka watendaji katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji kuwawezesha Watakwimu na Watehama katika taasisi wanazoziongoza kufanikisha ukusanyaji wa taarifa na takwimu za Sekta ya Maji wakati wote.

Waziri Aweso amesema hayo jijini Dodoma akifunga kikao kazi cha wataalam wanaohusika na takwimu na kuongeza kuwa hatua hiyo itawezesha taarifa na takwimu za Sekta ya Maji kuwa hai, na kuonyesha uhalisia.

Nikiri wazi kuwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kutoa takwimu na taarifa sahihi ni muhimu sana katika kuisaidia sekta yetu katika mipango na maamuzi yake mbalimbali ya masuala ya maji” – Aweso

Waziri Aweso amesema na kuongeza watendaji wa sekta ya maji wanatakiwa kuhakikisha wanasimamia masuala ya upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi za miradi ya maji ili kuiwezesha Serikali katika kutekeleza mipango yake.

Mhe. Aweso amesema uteuzi wa watalaam hao kufanya kazi hiyo umezingatia utekelezaji wa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ulioandaliwa na Wizara ya Maji (Integrated Water Sector Monitoring and Evaluation System – IWSMES) ambao ni mfumo unaobainisha majukumu ya kila taasisi katika utekelezaji wa masuala ya ufuatiliaji na tathmini katika sekta ya maji.

Waziri Aweso amezielekeza taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji ambazo ni RUWASA, Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira, Bodi za Maji za Mabonde na Maabara za Maji kuhakikisha zinatumia mfumo wa kielekroniki wa Maji Mobile Application (Maji App) kama chanzo rasmi cha takwimu za miradi ya maji. Pia, amezielekeza taasisi hizo kuandaa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kwa kuzingatia Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Sekta ya Maji.

Ameainisha kuwa Sekta ya Maji kwa muda mrefuimekuwa ikikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa takwimu zenye ubora na kwa wakati. Aidha, mifumo ya kielektroniki ya kukusanyia na kutunza takwimu kutoka idara na taasisi mbalimbali za Wizara ya Maji zimekuwa haziwasiliani.


Hivyo, Wizara ya Maji imeendelea kuboresha mifumo ya kielektroniki inayotumika kukusanya, kutunza na kuchakata takwimu za sekta ya maji ili kuifanya iwasiliane na miongoni mwa jitihada zilizofanyika ni kutengeneza mfumo wa kielektroniki wa Maji Mobile Application (Maji App) ambao unatumika kama chanzo kikuu cha takwimu za miradi ya maji hapa nchini.


Mfumo wa Maji App ulizunduliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Siku ya Maji Duniani, jijini Dar es salaam tarehe 22 Machi, 2022.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!