Na Ashrack Miraji
Taasisi isiyo ya kiserikali ya ”Utulivu” kwa kushirikiana na wizara ya Utamaduni, Sanaa na michezo inatarajia kuendesha matembezi maalum ya Utulivu mwishoni mwa mwa juma hili.
Akizungumza katika mkutano na Wanahabari mapema leo hii katibu mkuu wa Taasisi ya ”UTULIVU SPACE” Ndg; Mboni Kibelo amesema kuwa wamelenga kuandaa matembezi hayo ikiwa pia ni hamasa kuelekea kilele cha maadhimisho ya sherehe za Utulivu zinazotarajiwa kufanyika mnamo Septemba 14 mwaka huu.
”Sisi kama Utulivu tuligundua kuwa nchi yetu imebarikiwa vitu vingi vizuri lakini maarufu sana kwa ukarimu wa watu wake. Kwa kulitambua hilo tumeamua kuandaa jukwaa hili kwaajili ya kuyaenzi yale mazuri yaliyoasisiwa na baba wa taifa letu miaka ya nyuma kwenda kwa jamii ya kizazi cha sasa. Hivyo tumeamua kuja na Jukwaa hili la Utulivu kwaajili ya kufurahia Utulivu na Amani tulionao kama Taifa” Ameyasema hayo katibu Kibelo.
Kwa Upande wa wizara ya Utamaduni Sanaa na michezo, Afisa mwandamizi wa Sanaa , Ndg; Abel Ndaga naye amesema kuwa wameamua kushirikiana na Taasisi ya Utulivu kuandaa tukio hilo ikiwa ni kuunga mkono kwa juhudi zilizofanywa na waasisi wa taifa hili katika kuwaunganisha watanzania na kuwa kitu kimoja .
”Sisi kama wizara ya Utamaduni, Sanaa na michezo tumeamua kushirikiana na ndugu zetu wa Utulivu katika kuunga mkono yale ambayo viongozi wetu waliyaanza katika kutuunganisha watanzania kupitia Sanaa na michezo mbalimbali” Alisema mwandamizi Abel.
Aidha pia Mwandamizi Abel Ndaga ameongeza kwa kuwaomba watanzania kushiriki katika matembezi hayo kwani hayana ada ya ushiriki na pia kutakuwa na mfululizo wa shughuli mbalimbali za kiburudani zitakazokuwa zikiendelea siku hiyo.
Matembezi hayo yanatarajiwa kufanyika Jumamosi hii ya Julai 20 mwaka huu katika viwanja vya farasi (Green Grounds) vilivyopo Oysterbay Dar es Salaam ambapo yanategemewa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali na taasisi binafsi wakiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa