Na Shomari Binda-Bunda
JAMII imetakiwa kuacha vitendo vya kuwafanyia ukatili wa kijinsia wazee ili waweze pia kushiriki kuwalinda wasichana na watoto wa kike dhidi ya vitendo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa leo juni 15 kwenye uwanja wa shule ya msingi Miembeni mjini Bunda wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wazee na mkurugenzi wa shirika la Hope For Girls and Women Tanzania Robbi Samwel.
Katika maadhimisho hayo ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Mara Robbi amesema iwapo wazee wakifanyiwa ukatili nguvu ya utetezi dhidi ya wasichana na watoto wa kike itakuwa duni.
Amesema wazee wanahitajika katika mapambano ya kumlinda msichana na mtoto wa kike kwenye matokeo hatarishi yakiwemo ya ukeketaji.
Robbi amesema palipo wazee wapo wazee wa mila na desturi ambao wanayo dhamana kubwa ya kuzuia vitendo vya ukeketaji.
Mkurugenzi huyo ambaye shirika lake limekuwa likiwapokea watoto wa kike wanaokimbia vitendo vya ukeketaji na kuwahifadhi na kuwatunza kwenye nyumba salama zilizopo Serengeti na Bunda amesema wazee ni hazina wanatakiwa kulindwa.
Aidha Robbi amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwajali wazee hasa kuboresha kikokotoo kwa wastafu kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025 iliyosomwa bungeni.
Kwa upande wao wazee walioshiriki maadhimisho hayo wamesema jamii inapaswa kuungana kupinga ukatili wa aina yoyote dhidi ya wazee.
Mmoja wa wazee hao kutoka mkoani Pwani Waziri Hamza amepongeza maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee mkoa wa Mara na mapokezi waliyoyapata.