Na. Faustine Gimu, Elimu ya Afya kwa Umma.
Wazazi wameaswa kuweka msukumo wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana walioko shuleni ili kuwajengea afya imara na kuepusha mimba za utotoni na mimba zisizotarajiwa.
Wito huo umetolewa mkoani Morogoro na Afisa wa mpango wa afya shuleni kutoka Wizara ya Afya, Magdalena Dinawi katika kikao kilichoandaliwa na wizara ya afya cha kujadili mpango wa kusogeza mahusiano na mawasiliano ya afya ya uzazi baina ya mzazi na mtoto kilichokutanisha wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini ,asasi za kiraia,taasisi zilizochini ya Wizara ya afya pamoja na wizara za kisekta ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii,jinsia ,wanawake na makundi maalum pamoja na Wizara ya Elimu.
Dinawi amesema ni jukumu la kila mzazi kutoa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi kwa vijana balehe kwani pamekuwepo na changamoto ya kutopata taarifa muhimu kuhusu masuala ya afya ya uzazi kwa vijana .
“Ni jukumu letu kama wazazi na walezi kutoa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi kwa vijana balehe kwani kuna changamoto nyingi ikiwemo kukosa taarifa kuhusu mabadiliko ya mwili na changamoto ya ongezeko la vichocheo ndani ya mwili hali ambayo inaweza kumpelekea kijana kujiingiza kwenye vitendo hatarishi vinavyoweza kumsababishia madhara ikiwemo mimba za utotoni pamoja na maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI” amesema.
Kwa upande wake mkufunzi wa kitaifa wa afya ya uzazi kwa vijana Dkt.Taramael Ndossi amesema katika ulimwengu wa sasa kuna changamoto ya vijana kukosa malezi ya wazazi kutokana na muda mwingi kuutumia shuleni hivyo mpango wa elimu ya afya ya uzazi shuleni utasaidia kuelimisha wazazi na walimu namna nzuri ya kuwapatia elimu ya afya ya uzazi vijana walioko shuleni.
“Mtoto anakaa bweni anakulia bweni ,kwa hiyo huu mpango wa elimu wa afya shuleni umekuja na wazo kuwa kumbe tunaweza tukaelimisha wazazi,tukaelimisha na walimu na kuwafundisha mbinu za mawasiliano ili waweze kuwasiliana na vijana wetu kuhusu afya ya uzazi”amesema.
Kwa upande wao baadhi ya wawakilishi kutoka wizara za kisekta akiwemo afisa maendeleo ya jamii mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii ,jinsia,wanawake na makundi maalum Victor Rugarabamu amesema mtu wa kwanza mwenye jukumu la malezi kwa mtoto ni mzazi huku mwakilishi kutoka wizara ya Elimu Joel Mwamasangula akisema wazazi hawapaswi kujisahau suala la malezi wanapowapeleka watoto shule.
MWISHO