Na Shomari Binda-Musoma
WAVUVI katika jimbo la Musoma vijijini wameishukuru serikali chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mikopo nafuu kwaajili ya uvuvi wa vizimba.
Shukrani hizo zimetolewa na wavuvi was Kitongoji cha Busumi kilichopo Kata ya Suguti leo agosti 20 mara baada ya kufanikiwa kuingiza majini vizimba 4
Kupitia kikundi chao kilichopo chini ya Busumi Fishing Cooperative Society (Chama cha Ushirika cha Wavuvi wa Kitongoji cha Busumi) kimechukua mkopo nafuu usiokuwa na riba kutoka serikalini kwa ajili ya uvuvi wa vizimba ndani ya Ziwa Victoria.
Ushirika huo wa wanachama 20 umekopa shilingi milioni 117 kwa ajili ya kupata vizimba vinne (4), vifaranga vya samaki, chakula na bima ya ufugaji wao wa samaki.
Mmoja wa wavuvi hao aliyejitambulisha kwa jina la Mkama Maiga amesema wanaamini baada ya kuwezeshwa na serikali wanakwenda kunufaika kupitia uvuvi.
Maiga amesema serikali imewashika mkono nao watahakikisha wana simama imara katika kufanya shughuli zao ili kujiinua kiuchumi
Amesema wataalamu wa usukaji wa vizimba wamekamilisha kazi zao na tayari vizimba vilipelekwa ndani ya maji (Ziwa Victoria) eneo la Kijijini Suguti.
” Tunaishukuru sana serikali kwa mikopo hii ya vizimba kwaajili ya uvuvi na tuna amini imekuja kutuondoa kwenye umasikini kwa kutuinua kiuchumi”,amesema Maiga.
Uvuvi wa vizimba kwa upande wa jimbo la Musoma Vijijini, umeanza kwa mafanikio mazuri maeneo ya Vijiji vya Kigera (Etuma), Bwai Kwitururu na Suguti huku wavuvi wa maeneo mengine wamehamasika na wanajitayarisha kutuma serikalini maombi ya mikopo ya uvuvi wa vizimba