Katibu Mkuu Madini aanza Utekelezaji Maazimio
Kahama
Timu ya Watumishi wapatao 13 kutoka kada mbalimbali za Wizara ya Madini ikihusisha Makatibu Mahususi, Watunza Kumbukumbu na Wahudumu wametembelea Mgodi wa Barrick – Bulyanhulu uliopo Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio na ahadi alizotoa Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo lililofanyika mwezi Mei, 2023, jijini Dodoma.
Aidha, ziara hiyo inalenga kuwajengea uelewa wa pamoja watumishi wote wa Wizara kuhusu shughuli zinazofanywa katika Sekta ya Madini hususan shughuli za uchimbaji wa madini katika migodi mikubwa, ya kati na midogo ili kuwezesha malengo mahususi ya wizara kutekelezwa kwa pamoja kama familia moja ya Madini.
Watumishi hao wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali katika mgodi huo ikiwemo mgodi wa chini ( underground mining), sehemu ya uchenjuaji (processing plant) bwawa la huifadhi tope sumu ( TSF) , sehemu ya upokeaji na utunzanji wa vifaa vinavyotumika katika mgodi pamoja na kutembelea miradi ya jamii inayotekelezwa na migodi hiyo kupitia Mpango wa Uwajibikaji wa Migodi kwa Jamii (CSR).
Hili ni kundi la kwanza la watumishi wa kada hizo kutembelea maeneo ya migodi ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa. Kundi lingine la watumishi kutoka kada hizo linatarajiwa kutembelea migodi mbalimbali mapema mwezi Septemba.