Watu watano wakiwemo waendesha bodaboda na wakina mama wachuuzi wa bidhaa za matunda , mbogamboga na viungo kando ya barabara ya Boma, jirani na kituo kikuu cha zamani cha daladala mjini Morogoro wamejeruhiwa, watatu kati yao vibaya baada ya gari aina ya Canter kuacha njia na kuwaparamia.
Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Morogoro mkaguzi, Emmanuel Ochieng akizungumza eneo la ajali amekiri kupokea taarifa za uokozi majira ya saa moja usiku na kufika eneo la tukio ambapo majeruhi hao wamepelekwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa Morogoro kwa matibabu.
Katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Muuguzi wa zamu Asteria Bondo amebainisha kuwapokea majeruhi hao watano ambao wameumia zaidi maeneo ya kichwani na miguu na wanaendelea kupatiwa matibabu.
Mkuu wa wilaya ya Morogoro Albert Msando aliyefika eneo la ajali na baadaye hospitali akiongozana na kamati yake ya ulinzi na Usalama pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo kuwajulia hali majeruhi, alisema ajali hiyo imetokea wakati tayari asubuhi walikutana na baadhi ya Viongozi wa soko la Kingalu na wamachinga na kukubaliana wakutane jumapili kupanga namna
ya kuwaondoa watu wanaoendesha biashara maeneo yasiyoruhusiwa.