Home Afya WATU 267, 261  WAFIKIWA NA KAMPENI YA ELIMU NA UHAMASISHAJI CHANJO YA...

WATU 267, 261  WAFIKIWA NA KAMPENI YA ELIMU NA UHAMASISHAJI CHANJO YA SURUA 

Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Katika utekelezaji wa  agizo la  Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu la kuhakikisha  kuanzisha kampeni ya   Hamasa na Elimu kwa jamii umuhimu wa chanjo ya Surua, jumla ya watu 267, 261 wamefikiwa na elimu hiyo  Wilayani Mlele  mkoani Katavi   kwa njia ya magari ya matangazo na kwa njia ya sinema huku watoto 43,384 wakipatiwa chanjo ya Surua.

Hayo yamebainishwa Halmashauri ya Mpimbwe Wilayani Mlele  Mkoani Katavi na Afisa Programu  Elimu ya Afya kwa Ummma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Simon Nzilibili wakati wa kuhitimisha kampeni ya siku 14 ya Elimu na Uhamasishaji wa chanjo ya Surua iliyoendeshwa kwa njia ya magari na njia ya simena iliyoanza Febururi 24.2023 hadi Machi 9 2023 ikiwa ni utekelezaji wa kampeni hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Elimu ya Afya kwa Umma,Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Dkt.Haonga , Bw.Nzilibili amesema katika kipindi cha takriban wiki 3, wawakilishi kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Timu za Afya za Halmashauri na Mkoa wamefanikiwa kufikia wananchi wengi na kuhamasika wazazi na walezi kuwapeleka watoto kupata chanjo.

Katika kampeni hii ya kutoa elimu na kuhamasisha chanjo ya Surua kwa njia ya magari ,njia ya sinema  na kampeni ya nyumba kwa nyumba  tumeweza kufikia watu 267, 261 na hii imesaidia sana wazazi na walezi wengi kuwa na hamasa”amesema  Nzilibili.

Kuhusu takwimu za  chanjo  ya Surua, Nzilibili amesema jumla ya watoto 43,384 wamepata chanjo ya Surua katika Halmashauri  ya Mpimbwe Wilayani Mlele Mkoani Katavi.

Kwa watoto ambao tuliona hali zao sio nzuri tuliwabeba kwenye magari, jumla ya Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii 110 tulisaidiana nao  na mkakati mwingine ni upigaji wa mbiu ambapo tumefanikiwa kuchanja watoto 43,384 katika halmashauri ya Mpimbwe na mwitikio ulikuwa mkubwa sana na kila sehemu sinema ikioneshwa idadi ya uchanjaji iliongezeka mara mbili kabla ya sinema kuoneshwa” amesisitiza Nzilibili.

Hata hivyo,Nzilibili amewapongeza viongozi wote kuanzia serikali za mitaa hadi mkoa kwa kuonesha ushirikiano mkubwa katika kufanikisha zoezi hilo .

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mpimbwe Catherine Mashalla  ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuweka nguvu katika suala la elimu na uhamasishaji wa chanjo ya Surua kwani hatua hiyo imesaidia kuvuka lengo la Halmashauri ambapo walikuwa na lengo la kuchanja watoto 29, 000 lakini kutokana na hamasa hiyo  wamechanja watoto  43,384.

Nina shukuru sana kama Halmashauri tumepata Support ya kutosha kabisa kutoka Wizara ya Afya na kwa maana hiyo sasa tumeweza kufikia mafanikio haya hata ile trend ya kesi mpya nayo imeshuka leo tunazungumzia 56 kutoka mia na zaidi kuna maendeleo makubwa, wale wanaokwenda kulazwa sasa hivi tuna namba tu ya watu wawili, hata wale tuliowalenga halmashauri kuwachanja walikuwa ni 29,000  leo hii tunazungumzia  zaidi ya elfu arobaini na tatu ni mafanikio makubwaamesema Mashalla.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Halmashauri ameomba nguvu kubwa iliyotumika  katika elimu  na hamasa ya chanjo ya  Surua itumike pia katika  uhamasishaji kwa jamii kuhusu masuala ya lishe ili kupunguza tatizo la udumavu na utapiamlo katika eneo halmashauri ya Mpimbwe na Katavi kwa Ujumla.

Mganga Mkuu Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi Martin Lohay amesema watu waliogundulika na maambukizi ya Surua katika halmashauri hiyo ni   1967 huku akiipongeza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkoa pamoja na Wizara ya Afya kwa kusaidia katika utoaji wa elimu na hamasa ya chanjo ya Surua.

Ikumbukwe kuwa katika kampeni ya siku 14 ya Hamasa  ya chanjo na Elimu ya Surua Halmashauri ya Mpimbwe, jumla ya kaya 15,750 zilitembelewa, na magari ya matangazo na sinema kufika katika maeneo ya  Majimoto, Kibaoni, Chamalendi, Mbende,Mwamapuli, Kasansa, Usevya, Ikuba, na Mamba huku watoto waliopona Surua ni 1749 kati ya wagonjwa  1967 na waliofariki hadi sasa ni watoto 16.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!