Na Mathias Canal, WEST-Dodoma
Serikali imesema kuwa wathibiti ubora wa elimu ni mboni ya serikali katika kusimamia na kuimarisha ubora wa elimu nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 29 Septemba 2022 Jijini Dodoma wakati akizungumza na wadhibiti ubora wa Kanda zote nchini.
Amewataka wathibiti ubora kote nchini kusimamia kwa weledi zaidi ubora wa elimu kwani wao ni moyo na injini ya elimu.
Waziri Mkenda amewataka wathibiti ubora kubadili mfumo wa kufanya kazi ambapo amewataka kutoa taarifa mara kwa mara za kazi wanazofanya kila siku na changamoto zinazowakabili walimu na wanafunzi.
“Walimu wamerundikana maeneo ya mjini kuliko vijijini lakini katika maeneo yote hayo kuna watanzania wengi wanaohitaji elimu, kwa sasa jambo kubwa ambalo tunapambana nalo ni walimu wengi kutaka kuhama kutoka vijijini kwenda mjini” Amesisitiza Waziri Mkenda na kuongeza kuwa
“Walimu wengi hupambana kutafuta kazi na wakati wa maombi husema wapo tayari kufanya kazi popote lakini wakishaipata hiyo kazi ya ualimu wanaanza kupambana kuhama”
Amesema kuwa serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu ambazo ni pamoja na vitendea kazi na ubora wa madarasa.
Waziri Mkenda amesema kuwa wakati serikali inaendelea kufanya mageuzi ya elimu nchini ni vyema wathibiti hao wa ubora wa elimu kuhakikisha kuwa wanatoa maoni ya namna ya kuboresha vigezo na sifa za ubora wa elimu.
Prof Mkenda amesema elimu bora itapatikana na kuakisi mahitaji ya nchi endapo kama Maafisa Uthibiti Ubora watakuwa wanaharakati wa mabadiliko katika maeneo yao ya kazi.
Kadhalika ametoa kibali kwa walimu wanaoomba kwenda kusoma ambapo ametaka wapewe ruhusa ili kuongeza sifa na weledi katika utendaji kazi wao kwa kufuata taratibu na sheria za utumishi wa umma.
MWISHO