Na Neema Kandoro Mwanza
JESHI la Polisi Mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu Kwa Mauaji ya watu wanne Kwa Nyakati tofauti katika Wilaya ya llemela na Nyamagana jijini hapa Kwa vifo vya moto na kukatwa Kwa kitu chenye ncha Kali
Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Wilbroad Mtafungwa alisema kuwa Novemba 14 katika mtaa wa Kashishi Kata ya Nyamhongolo wilayani Ilemela Flora Philemoni (42) aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema chanzo cha kifo hicho ni kuwania mali ambapo Elizabeth Josephat maarufu kama Ndakubegi (35) mfanyabiashara mkazi wa Daressalaam na Faida Daud maarufu kama Mataba (24) mkazi wa Igoma wamekamatwa kwa nyakati kwa tuhuma za mauaji hayo.
Kamanda Mtafungwa alisema watuhumiwa wa mauaji hayo wamefikishwa mahakama ya wilaya ya Ilemela kujibu mashitaka yanayowakabili.
Wakati huohuo jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watu wawili kwa tuhuma za kuchoma nyumba na kusababisha vifo vya watu watatu wa familia ya Eva Stephano wa eneo la Lwanhima wilayani Nyamagana hapo Disemba 7.
Aliwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa Nestory John (52) mkazi wa Buhongwa wilayani Nyamagana aliyekamatiwa kwa mganga wa jadi Mkoani Geita pamoja na mganga wake Samson Mwinamila (35).
“Jeshi hili limejipanga kuimarisha ulinzi na usalama katika vipindi vya sikukuu zote na nawataka madreva kuendesha kwa kufuata sheria za usalama barabarani” alisema Mtafungwa.
Kufuatia kuelekea sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya Kamanda Mtafungwa amewataka wakazi Mkoani hapa kujiepusha na matukio ya kiuhalifu,unywaji pombe kupita kiasi na kuendesha magari kwa mwendokasi.