Na Theophilida Felician, Kagera
Jeshi la Polisi Mkoani Kagera limesema kuwa limefanikiwa kuwakamata watu watatu wakituhumiwa kushiriki mauaji ya watoto 7 wa familia moja huko Kijiji cha Nyakanazi wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera mnamo Tarehe 13, Novemba mwaka 2023.
Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa watu hao kwa waandishi wa habari ofisini kwake Manispaa ya Bukoba hii Leo Tarehe 23, Novemba mwaka huu wa 2023 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Kagera Blasius Z. Chatanda amesema kuwa watu hao walikamatwa wakiwa wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita walikokimbilia baada ya kutekeleza mauji ya watoto hao wa Mzee Razaro Sanabanka mkazi wa Kijiji hicho hicho cha Nyakanazi.
Amewataja watuhumiwa kuwa ni pamoja na Jenipher Petro Nyakidi mwenye umri wa miaka 19, mkazi wa Nyakanazi Mernes Petro miaka 22 naye Mkazi wa Nyakanazi na Emmanuel Julius Noel mkazi wa Masumbwe miaka 31.
Kamanda Chatanda amefafanua kuwa baada ya kuwakamata watuhumiwa walihojiwa nakukiri kuhusika na mauaji hayo yakikatili baada kuweka sumu kwenye mboga za majani ya maharage (Msogoro) kwa lengo la kulipiza kisasi kwa familia ya mzee Razalo kwatuhuma za kwamba watoto wa mzee huyo wameiba kuku wao mmoja jogoo nakwenda kumchinja.
Sumu hiyo aina ya BIAZION inayotumika kuua wadudu iliwaua watu saba na wengine 4 kujeruhiwa.
Waliofariki baada ya kutumia chakula chenye mboga hiyo iliyowekewa sumu ni Melisa Lazaro mwenye umri wa miaka 11, Melinas Lazaro miaka 9, Kahindi Samsoni miaka 9, Happynes Lazaro miaka 12, Brian Ezekiel miaka 3, Josephina Juma miaka5 na Meleciana Lazaro wote wakiwa wa familia moja ya Mzee huyo.
Kamanda huyo amesisitiza kuwa jeshi hilo litawafikisha mahakamani watuhumiwa kwa mjibu wa sheria kwa nia ya kuwatia hatiani ili wawaze kuadhibiwa vikali na liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia mbovu ya kutenda vitendo vya kikatili dhidi ya wenzao.
Amehitimisha akitoa onyo kali kwa watu wote watakaothubutu kushiriki vitendo vya uhalifu yakiwemo mauji kuacha mara moja kwani Jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua kali kwa wale watakaobainika kuhusika na matukio ya aina yoyote ya uhalifu huku akiwatakia wananchi Kheri ya sikukuu za Christmass na Mwaka mpya wa (2024)