Na Mwandishi wetu
BALOZI wa kujitolea wa Mazingira nchini Moses Mwakibolwa kutoka kampuni ya Orbit Environmental Consultancy ametoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya kupanga miti kama njia ya kulinda Mazingira hususani kwenye vyanzo vya maji nchini bila kusubiri maelekezo ya viongozi wa serikali
Ameyasema hayo jijini Dar Es Salaam wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu kampeni ya upandaji miti katika vyanzo vya mto Kilombero na Tindiga Wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro kuanzia tarehe 14/10/2022 ambapo miche ya miti 10,000 itapandwa katika maeneo hayo muhimu
“Hali ya ukataji miti nchini imekuwa kwa kasi sana na hivi karibuni viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa wito kila mmoja apande miti, hivi karibuni waziri mkuu mheshimiwa Kassim Majaliwa siku ya Mazingira duniani aliagiza ipandwe miche 1,500,000 nchini kote kutokana na uharibifu wa Mazingira na ukame” alisema
Balozi huyo wa kujitegemea amesema ifike wakati jamii kujenge tabia na kuweka utaratibu wa kupanda miti kwa hiyari kutokana na uharibifu mkubwa katika vyanzo vya maji ambako baadhi ya wakulima wamekuwa na tabia ya kukata miti kwa ajili ya mbao, mkaa lakini pia wanakata miti kwa ajili ya kulima mazao ya muda mfupi ambayo wakati mwingine hukosa tija na kuacha uharibifu mkubwa kwenye mabonde ya maji
Mwakibolwa ametoa mfano wa maeneo ya Kilangali na Tindiga ambako kuna bonde linalopitisha maji kwenda kwenye mbuga ya Mikumi lakini wakulima katika kata hizo Wilayani Kilosa wamekuwa wakichepusha maji bila kufuata utaratibu na kusababisha maji kupoteza mwelekeo, pia amewataka wakulima wa miwa bonde la Kilombero kushiriki katika kampeni hiyo endelevu kwa kuwa ina faida kubwa kwa bà adae kutokana na Kilimo cha miwa ambayo inahitaji maji ya kutosha
Aidha amewataka wadau wa misitu na Mazingira kutengeneza mahusiano na wakulima ili waweze kubadili tabia ya kuacha kulima mazao ya muda mfupi na kupanda miti ya matunda ambayo ina faida kubwa kwenye masoko na mavuno yake ni makubwa ukilinganisha na mazao mengine