WATANZANIA wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili waweze kupata mafanikio ya kiuchumi kutokana na shughuli wazifanya kwani serikali ya awamu sita imeboresha mazingira mazuri kwa ufanyaji biashara.
Hayo yamebainshwa na wadau wa maendeleo Jijini Mwanza walipokuwa wakizungumza na jana kufuatia mbio za mwenge kuwafikia katika maeneo yao kuweka mawe ya msingi na kuzinduzi miradi ya maendeleo.
Mkereketwa wa mbio za mwenge wa uhuru Bernard Kajuna wa Mkolani ambaye ni Mkurugenzi kituo cha uwekezaji Family Corner kinachojengwa jijini Mwanza eneo lilowekewa jiwe la msingi aliwataka watanzania kujituma ili waweze kujiletea maendeleo yao.
Alisema watanzania wanapashwa kuona fahari kushuhudia mbio za mwenge wa uhuru ambao ni kitu cha kipekee kinachotambulisha Utanzania wetu ndani na nje ya mipaka yetu kwa kufanya jitihada za kimaendeleo ambazo zitafanya miradi hiyo kufikiwa kwa ajili ya kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa kwa mbio hizo.
Alisema kwa sababu ya hamasa ambayo mbio za mwenge imekuwa ikifanya hapa nchini inatakiwa kuchochea wananchi kufanya kazi kwa bidii kwani yapo mazingira mazuri kwa mtanzania kutumia fursa za mabenki na taasisi za fedha katika kujiendeleza kiuchumi.
Baadhi ya madiwani katika manispaa ya Ilemela walisema kuwa wamefurahishwa kuona kuwa miradi mingi ya serikali iliyozinduliwa imetumia fedha zake yenyewe hivyo kuwasihi wananchi kufanya shughuli za maendeleo yao wapate mafanikio kwani serikali imefungua fursa nyingi za kiuchumi.
Diwani wa Kata ya Shibula Swila Dede aliwataka wananchi katika eneo lake kufanya kazi za kujiletea maendeleo kwani serikali imewajengea miundombinu wezeshi ya sekta ya elimu, afya na usafiri kwenye kata hiyo hivyo kuwaondolea wananchi mzigo wa kuchangia michango ya ujenzi wake.
Diwani wa Viti Maalum katika Manispaaa ya Ilemela Sarah Lisso alipongeza serikali kwa kuleta fedha za boost ambazo zimesaidia kuongeza vyumba vya madarasa katika maeneo mbalimbali wilayani pamoja na shule mpya hivyo kuwaondolea wananchi adha ya kuchangia ujenzi wake.