Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe ametoa rai kwa Watanzania kupenda na kunununua bidhaa zinazotengenezwa na viwanda nchini ili kupanua wigo wa masoko ya bidhaa, kuongeza uzalishaji kukuza viwanda, kuongeza ajira na kipato cha mtu binafsi na pato la Taifa.
Kigahe ameyasema hayo Oktoba 23, 2023 alipokuwa akifungua Maonesho ya nne (4) ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Sabasaba Mkoani Njombe kuanzia 21 – 31/ 10/2023 yakiongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Pamoja Tujenge Viwanda kwa Uchumi na Ajira Endelevu”.
Akihutubia katika ufunguzi huo, Kigahe ameielekeza SIDO kushirikiana na Halmashauri zote nchini kuzalisha kwa wingi teknolojia ili kukiwezesha kilimo kuwa cha kibiashara na chenye tija, kuwezesha kuchakata mazao ili yasiharibike na kuvutia vijana wengi kuingia katika sekta ya kilimo na viwanda.
Vilevile, ameielekelza Wakala wa Maendelo ya Viwanda Vidogo na vya Kati.(SMIDA) kushirikiana na SIDO katika kupata teknolojia na kuwawezesha vijana wa Zanzibar kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji ili nao waweze kuitumia fursa ya uwepo wa AfCFTA, EAC, SADC, AGOA na fursa nyingine za masoko ya pamoja.
Katika hatua nyingine, ameishauri SIDO kuendelea kuratibu Maonesho hayo Kitaifa kufanyika Mkoani Njombe kila mwaka kama ilivyo vya Sabasaba kitaifa kila mwaka ni Dar es Salaam , Dhahabu ni Geita kwa kuwa Maonesho hayo yanaonesha taswira nzima ya bidhaa za kitanzania, teknolojia. ubunifu, mafanikio na fursa kwa Mtanzania kutumia na kupanua wigo wa uzalishaji.
“Serikali inaendelea kufungua mipaka ya kuuzia bidhaa za mazao yetu hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunafanikisha kuunganisha sekta za uzalishaji za Kilimo, Mifugo, Maliasili, Uvuvi na viwanda vya kuchakata na teknolojia ambayo vinarahisisha uzalishaji na uwepo wa soko la uhakika kwa mazao yatakayo ongezwa thamani.” Amesema Kigahe
Kigahe pia amehimiza uanzishwaji wa viwanda vya aina tofauti kulingana na mahitaji pamoja na kutumia teknolojia ili kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao na bidhaa zenye ubora na tija ili kuhimili ushindani katika soko na kulilisha soko la ndani na nje ya nchi .
Naye Mkurugenzi Mkuu wa SIDO Mha. Prof. Sylvester M. Mpanduji amesema Maonesho hayo hutoa kwa wajasiliamali kukutana pamoja, kujifunza, kubadikishana uzoefu na kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta njia sahihi za kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili