Waziri wa Madini Mh. Anthony Peter Mavunde amewataka wamiliki Leseni za madini nchini kuziendeleza leseni husika kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza kwa kuwa zipo leseni nyingi ambazo hazifanyiwi kazi na hivyo kuzorotesha ukuaji wa kasi wa sekta ya madini.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Wilayani Ruangwa,Lindi wakati alipotembelea Mgodi wa Madini Kinywe wa Lindi Jumbo ambao unatarajia kuanza uzalishaji mwishoni mwa mwezi Machi,2024.
Akitoa taarifa ya Mradi,Meneja Msimamizi wa Mradi Mhandisi Chediel Mshana amesema ujenzi wa mgodi huo umefikia 90% na kwamba ifikapo mwezi Machi,2024 mgodi utakuwa umeanza uzalishaji rasmi wa madini ya kinywe.
“Ninawapongeza Lindi Jumbo kwa hatua kubwa ya ujenzi ulipofikia na ahadi ya kuanza uzalishaji rasmi wa madini mkakati haya mapema mwaka 2024.
Huu utakuwa kati ya miradi michache mipya ya uchimbaji wa madini mkakati ya kinywe nchini Tanzania ambao utakuwa umeanza hivi karibuni.
Ni dhamira ya serikali chini ya uongozi wa Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona shughuli za uchimbaji wa madini zinaongezeka ili kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na kuleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi na kuongeza nafasi za ajira.
Nitumie fursa hii kuwatangazia wale wamiliki wa Leseni wasiondeleza maeneo yao kuzingatia matakwa ya sheria juu ya umiliki wao wa leseni husika vinginevyo leseni hizo zitafutwa kwa mujibu wa sheria na kutoa nafasi ya watu wanaoweza kuendeleza,kwa kuwa kwa hivi sasa wapo watu wengi wanashikilia maeneo makubwa ya madini pasipo kuyafanyia kazi na kuwanyima fursa watu wengi zaidi kushiriki katika uchumi huu”Alisema Mavunde
Naye Mkuu wa Wilaya wa Ruangwa Mh. Hassan Ngoma amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea ukuaji wa sekta ya madini na maendeleo katika wilaya hiyo kuahidi kufanyia kazi changamoto ya barabara inayoenda mgodini hapo ili kurahisisha shughuli za uchimbaji madini.