
Michuano ya KITILA JIMBO CUP imehitimishwa January 02, 2025 kwa Timu ya Wima kutoka Kata ya Mburahati kushika nafasi ya kwanza na kukabidhiwa zawadi ya Bajaji na Kombe baada ya kuishinda Timu ya Baruti kutoka Kata ya Kimara Bao 3 kwa 1.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Timu ya Baruti waliopatiwa zawadi ya Pikipiki huku Timu ya Kimara Combine ikijipatia kitita cha Sh. Milioni 1 baada ya kushika nafasi ya tatu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo Mbunge wa Jimbo la Ubungo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema aliamua kuandaa mashindano hayo ili kuamsha morali ya michezo kwa vijana.
Kuhusu zawadi walizokabidhiwa washindi ambazo ni Bajaji kwa mshindi wa 1 Pikipiki kwa mshindi wa 2 na fedha taslim Sh. Milioni 1 Prof. Kitila amesema aliamua kuandaa zawadi hizo ili kuchochea Uchumi kwa wachezaji maana watakuwa na chanzo cha kipato.

Awali Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema wapo mbioni kuufanya uwanja wa Kinesi kuwa chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ili uweze kufanyiwa ukarabati unaostahili.
Amempongeza Prof. Kitila Mkumbo kwa kuendesha mashindano hayo na kutoa zawadi kubwa kwa washindi huku akiwataka wakazi wa Jimbo la Ubungo kumshikilia Mbunge huyo.

“Nikupongeze kwa kuandaa mashindano haya, inaonyesha ni kwa namna gani unawajali vijana ambao ndiyo wahusika wakubwa wa michezo” alisema Mwinjuma
“Mimi nisingekuwa Mbunge ningekuwa ni Mpiga kura ningependa kuwa na Mbunge wa aina ya Prof. Kitila Mkumbo” alisema Naibu Waziri huyo.
Mashindano ya KITILA JIMBO CUP yalihusisha Timu 16 ambapo kila Kata ilitoa Timu mbili.
Mwisho