Home Kitaifa WARATIBU WA MAFUNZO YA TEWW WANOLEWA USIMAMIZI, UENDESHAJI WA MAFUNZO YA ELIMU...

WARATIBU WA MAFUNZO YA TEWW WANOLEWA USIMAMIZI, UENDESHAJI WA MAFUNZO YA ELIMU YA SEKONDARI KWA NJIA MBADALA

Na Timoth Anderson

Waratibu wa mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP-AEP) wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) wamekutana mkoani Morogoro kwa lengo la kujengewa uwezo katika kuboresha usimamizi na uendeshaji wa programu hizo.

Mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku nne katika Kampasi ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Morogoro (WAMO), yamefunguliwa tarehe 25 Machi, 2024 na Meneja wa Kampasi hiyo, Dkt. Honest Kipasika akimwakilisha Mkuu wa TEWW, Prof. Michael Ng’umbi.

Dkt. Kipasika amewataka waratibu hao kufuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizoandaliwa na kutoa maoni yao na hatimaye kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utolewaji wa elimu ya Sekondari kwa njia Mbadala ili kuwezesha kupata matokeo chanya yaliyokusudiwa na mradi.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na TEWW na yamepangwa kuwafikia waratibu wote wa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala.

Mwakilishi wa waratibu wa mafunzo kutoka Kanda ya Ziwa, Ndugu Peter Frank ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shule Huria ya BSL, ameshukuru uongozi wa TEWW kwa kuandaa kikao kazi hicho ambacho amesema kitatumika kama sehemu muhimu ya kupeana mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za utoaji mafunzo zinazofanyika kwenye vituo vya Elimu ya Watu Wazima katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

“Mafunzo haya yatatoa nafasi ya kupeana mrejesho na uzoefu wa utekelezaji wa shughuli za utoaji mafunzo ili kuleta ufanisi katika mafunzo yanayotolewa na TEWW,”amesema.

Aidha, Mratibu wa Mradi wa SEQUIP kutoka TEWW, Ndugu. Baraka Kionywaki, amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia washiriki kuongeza uelewa na namna bora ya kuwadahili, kuwafundisha na kuwasimamia wanafunzi ili kuwezesha ufaulu mkubwa katika mitihani ya kidato ya pili na kidato cha nne.

 Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa kwenye warsha hiyo ni mafanikio ya Mradi wa SEQUIP-AEP, majukumu ya waratibu wa Mradi, ufuatiliaji na tathmini ya mafunzo, uzoefu wa waratibu wa Mradi kuhusu changamoto na namna wanavyokabiliana nazo katika kutekeleza mradi huo pamoja na  matumizi ya mfumo wa taarifa za shule ‘SIS’.

Mafunzo hayo yamehusisha waratibu takribani 80 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara ambao ni wakuu wa shule, maafisa elimu kata na waalimu ambao wanaratibu mradi wa SEQUIP-AEP ambao Serikali ya Awamu ya sita ilitoa fursa ya pili ya kurudi shuleni kwa mabinti ambao walikatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwepo ugonjwa, hali ngumu za Maisha na ujauzito.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!