Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Abdul Kitungi amewataka Vijana waongoza Watalii wilayani Mafia kulinda maadili ya kitanzania katika kuwahudumia Watalii wanaofika kumtembelea kujionea utalii uliopo kisiwani humo..
Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) kwa kushirikiana na Shirika linalojihusisha na Uhifadhi wa Mazingira na Utunzaji wa Papa Potwe (WATONET), Chuo cha Taifa cha Utalii pamoja na Taasisi ya TACCI yamelenga kuchagiza shughuli za utalii wilayani Mafia na kuwatengenezea ajira vijana.
Amesema kuongoza Watalii ni ajira muhimu lakini lazima izingatie taadhali ya kulinda na kuhamasisha maadili ya kitanzania.
“Nyinyi waongoza Watalii ndio kundi la kwanza kuelekeza Watalii maadili yetu ni yapi muwaongoze kuyalinda katika shughuli zenu za kila siku” alisema Kitungi.
“Waongoza watalii wana nafasi kubwa sana kwenye kuutangaza utalii, kwa sababu wao wanatoa huduma na kuwapokea wageni”.
Aidha, amewataka vijana hao kutumia fursa hiyo kuitangaza Mafia katika utalii na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukuza sekta ya utalii nchini.
Mtendaji Mkuu wa Shirika la WATONET, Juma Salum amesema Vijana 30 wilayani Mafia wamepatiwa mafunzo ya uongozaji wa watalii pamoja na sanaa ya ngoma za asili yaliyolenga kuwajengea uwezo katika masuala ya utalii ilikuongeza weredi wa utandikaji Kazi wao.
“Tukiwa na waongoza watalii ambao hawana weledi na taaluma, taswira ya eneo ambalo watalii wanakuja inakuwa si nzuri”
“Hii ni awamu ya pili ya utoaji wa mafunzo hayo ambapo kwa mwaka 2023, vijana 25 kutoka kata 6 walishiriki mafunzo ya uongozaji utalii pekee kwa kulinganisha na mwaka huu 2024 ambapo Shirika la WATONET limetanua wigo kwa kuongeza mafunzo ya ngoma za asili ambayo yalitolewa mkoani Morogoro na taasisi ya TACCI”.
” Tunaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kutoa kibali cha mafunzo hayo, pamoja na Shirika la WWF na WATONET kwa kushirikiana na wakufunzi wetu kwa kutupa mafunzo haya”.
“Tunaomba kutambuliwa rasmi wilayani kwa kupata vitambulisho ili tuweze kutambulika kisheria na kutunza ajira zetu” alisema Amini Abdallah, kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo ya waongoza watalii