Home Kitaifa Wanawake wakumbushwa kutosahau Jukumu lao la Msingi la Malezi

Wanawake wakumbushwa kutosahau Jukumu lao la Msingi la Malezi

Mtandao wa Polisi Wanawake wa Jeshi la Polisi (TPF-Net) Mkoa wa Mwanza umewataka wanawake wafanyabiashara wa Samaki katika Soko la Kamanga Jijini Mwanza kutosahau majukumu ya msingi ya malezi wakati wanapotekeleza wajibu wao wa kutafuta kipato cha familia.

Wito huo umetolewa leo Machi 5, 2024 na Mwenyekiti wa Mtandao huo Mkoani Mwanza, Mrakibu wa Polisi (SP) Virginia Sodoka, wakati wanachama wa mtandao huo walipotembelea na kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake wajasiriamali kuelekea maadhimisho ya ‘Siku ya Wanawake Duniani’.

Mrakibu Sodoka ambaye pia ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana amesema tabia za wanawake wajasiriamali kujitafutia kipato ‘fedha’ na kusahau
wajibu wao katika malezi ya familia kinachangia familia kusambaratika jambo linalohatarisha usalama na kupelekea watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili.

“Hizi pesa tunatafuta kwa shida tuwe makini, pata pesa yako badili maisha ya familia yako ili familia ifurahie uwepo wako na utapata baraka” amesema.

Awali, Mkuu wa Kituo kidogo cha Polisi Mirongo jijini Mwanza, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (A/Insp) Fatuma Mpinga alifafanua (bila kutaja idadi)
kwamba visa vingi vya watoto kufanyiwa ukatili ikiwemo kubakwa na kulawitiwa huchangiwa na wazazi kutotenga muda kuwachunguza na
kufuatilia mienendo ya watoto wao.

“Wakina mama tusiwe wasiri kwenye hili, sisi tunachangia watoto wetu kuna vitu wanafanyiwa na wakina baba sisi hatutoi taarifa hata kama tunawapenda sana wakina baba lakini tuangalie na watoto kwani ndio Taifa la kesho“

Mfanyabiashara wa samaki katika soko la Kamanga jijini humo, Bi. Veronica Charo amekiri kuwepo wajasiriamali wanaojisahau na kutelekeza
familia jambo linalotengeneza mazingira hatarishi kwa watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kubakwa na kulawitiwa.

“Tunavyoona wale watoto wa mitaani wanavyoishi tunajisikia vibaya; mtoto wa mwenzako ni wa kwako, unapoona amepata changamoto unaumia katika nafsi” amesema Veronica

Aidha, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mwanza, Insp Faraja Mkinga amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vimepungua kutokana na jamii kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa fiche za uhalifu.

“Endeleeni kutoa taarifa Polisi za vitendo vya ukatili wa kijinsia; acheni kumaliza kesi hizo kifamilia majumbani kwani mnawaumiza watoto wenu“

Naye, Mfanyabiashara katika soko hilo Lilian Charles, amesema baadhi ya wanawake huwatendea waume zao ukatili ikiwemo wa kuwanyima unyumba kwa madai ya kuchoka kutokana na shughuli walizofanya siku nzima.

“Mliyosema ni kweli lakini wanaume nao wananyanyasika na sisi wanawake wapo wanaowanyanyasa wanaume, muitishe kikao na wanaume nao watoe kero zao ni basi tu wao wanaishi kwa ujasiri lakini wana changamoto sana maana mwanamke anapotoka kwenye majukumu yake hataki kuguswa na mwenza“

TPF Net mkoa wa Mwanza inaendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusiana na ukatili wa kijinsia na ulinzi shirikishi katika jamii ambapo mbali na kujengewa uwezo na uelewa, wananchi wanatakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kukomesha vitendo vya Uhalifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!