Home Biashara Wanawake wafanyabiashara watakiwa kushiriki Kongamano la Wanawake la AfCFTA 2023

Wanawake wafanyabiashara watakiwa kushiriki Kongamano la Wanawake la AfCFTA 2023

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zenna Ahmed Said, ametoa wito kwa wanawake wote wanaojihusisha na biashara kushiriki Kongamano la Pili la Wanawake katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) linalotarajiwa kufanyika tarehe 06 hadi 08 Disemba, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Kiongozi huyo amayasema hayo Novemba 30,2023 akiwa katika kikao cha maandalizi ya Kongamano hilo ambalo Tanzania ni mwenyeji na linaandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Sekretarieti ya AfCFTA na linaongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Kuimarisha Ushiriki wa Wanawake katika Biashara na Kuongeza Kasi ya Utekelezaji wa AfCFTA”

Aidha, Alisema kuwa kongamano hilo ni fursa muhimu kwa wanawake wafanyabiashara kutoka Tanzania na Afrika kupata maarifa, ujuzi na ushirikiano kutoka kwa wataalamu na wadau mbalimbali kutoka duniani kote.

Amesema Kongamano hilo pia litakuwa fursa muhimu kwa wanawake wafanyabiashara kubadilishana uzoefu na kushiriki mikakati ya kuimarisha ushiriki wao katika biashara ndani ya Afrika na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Kongamano hili linalenga kuwakutanisha pamoja wanawake katika biashara kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika biashara. Hivyo, changamoto mbalimali ambazo wanawake wanakabiliana nazo zitajadiliwa pamoja na njia ya kuzitatua ili waweze kunufaika ipasavyo na fursa za biashara zinazotokana na Mkataba wa AfCFTA,” alisema Mhandisi Zenna.

Vilevile, Katibu Mkuu Kiongozi huyo alieleza kuwa wanawake ni kiini cha biashara na wamekuwa chachu muhimu katika maendeleo ya uchumi duniani, hivyo wanatakiwa kujumuishwa ili kuchangamkia fursa zinazotolewa chini ya Mkataba wa AfCFTA.

Aliwataka wanawake wafanyabiashara kujisajili kwa ajili ya kushiriki kongamano hilo kupitia anuani ya tovuti https://au-afcfta.org/wit/. Link hii pia inapatikana kupitia tovuti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ni www.viwanda.go.tz

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!