Na Shomari Binda-Bunda
MKUU wa Mkoa wa Mara Said Mtanda ametoa wito kwa wanawake wa mkoa wa Mara na nchi nzima kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hadi 2025.
Wito kwa wanawake hao ameutoa kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoadhimishwa kimkoa Kata ya Nyamswa wilayani Bunda.
Amesema Rais Samia amewaheshimisha wanawake kwa uongozi wake thabiti na wenye mafanikio hivyo wanapaswa kumuunga mkono.
RC Mtanda amesema wanawake watembee na Rais Samia kuanzia sasa kwa kumsemea mazuri anayofanya hadi uchaguzi wa mwaka 2025.
Amesema wanawake ni jeshi kubwa na wakiamua jambo lao lazima lifanikiwe na hata maadhimisho ya siku yao kwa mkoa wa Mara yamefanikiwa.
“Niwapongeze kamati ya maandalizi ya shughuli yenu wanawake wa mkoa wa Mara kwa kweli mmefanikiwa na sherehe imefana”
“Pili nitoe wito kwenu na kuwaomba kutembea na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hadi 2025 na aweze kupata mitano tena” amesema
Aidha mkuu huyo wa mkoa amesema yeyote atakayetaka kuvaa Rais Samia watashughulika naye hadi kieleweke na kushinda tena.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM mkoa wa Mara Nancy Msafiri amesema watamuunga mkono Rais Samia kwa kuwa uongozi wake ni imara na kazi alizofanya zinaonekana.
Kwa upande wake Mjumbe wa jumuiya hiyo Taifa kutoka mkoa wa Mara Mbaraza Rhobi Samwel amesema Rais Samia ameleta fedha nyingi mkoa wa Mara na anaendelea kuleta kwaajili ya miradi mbalimbali hivyo lazima watatembea nae hadi 2025.