Home Kitaifa Wananchi walia na mgawo wa Maji

Wananchi walia na mgawo wa Maji

Na Neema Kandoro, Mwanza

WANANCHI katika mtaa wa Buhongwa Mashariki wameiomba Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mkoani Mwanza (MWAUWASA) kuwapunguzia mgawo wa maji kutoka wiki moja kwani hali hiyo inawaongezea gharama za kimaisha.

Wakizungumza Leo wananchi hao walisema kuwa wamekuwa wakipata mgawo wa maji kwa wiki moja lakini kwa sasa muda huo umekuwa ukipita bila kupata huduma na kuwafanya kununua ndoo ya maji kwa sh. 500.

Mkaazi wa Mtaa wa Buhongwa Gaudencia Kwangu aliomba mamlaka hiyo kuzingatia ratiba ya mgawo wa maji katika eneo lao ili kuwaepushia usumbufu unaotokana na uhaba wa unaojitokeza mara kwa mara.

Mkurugenzi wa Lovebless Bakery Lucas Luhunga alisema kuwa wanakabiliana na adha ya upungufu wa maji na hivyo kuwalazimu kununua bidhaa hiyo kwa bei kubwa hatua ambayo inachangia ongezeko la gharama ya uendeshaji wa kazi yao.

Aliomba mamlaka kuwasaidia kupatikana maji kwa mgawo uliopangwa eneo hilo ili kuwawezesha kufanya shughuli zao bila ya kuwepo kwa ongezeko linalosababishwa na kutokufuatwa kwa ratiba ya mgawo.

Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Buhongwa Mashariki Simon Dollo alisema wamekuwa wakikabiliana na tatizo la uhaba wa maji licha ya kuwepo kwa mgawo siku ya Alhamisi au Ijumaa lakini kwa sasa inaweza kupita wiki bila ya kupata huduma hiyo.

Dollo aliomba serikali kuharakisha kujenga miundombinu ya maji toka chanzo cha maji Butimba ili kuwaondolea adha hiyo na vilevule kufuata ratiba ya mgawo ili kuwaepushia wananchi na adha ya upatikanaji wa maji.

Diwani wa Kata ya Buhongwa Joseph Kabadi alisema kuwa ni kweli wananchi wanakabiliana na mgawo wa umeme hata hivyo alisema kubadilishwa kwa muda wa mgawo waweza kufanywa na watumishi wasio kuwa waaminifu kutoka MWAUWASA.

Alisema hata hivyo suala la changamoto ya maji katika maeneo hayo linaweza kuisha pale mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo cha Butimba litakapo kamilika baada ya kuwa imefikia zaidi ya asilimia 85.

Mkurugenzi wa MWAUWASA hakuweza kupatikana licha ya simu yake kuita bila ya kupokelewa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!