Na Mwandishi wetu
Serikali kupitia Wizara ya Maji imeahidi kuchimba kisima na kujenga tenki la maji kwa wananchi wa kijiji cha Nyabu na Seluka katika jimbo la Kibakwe Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa waliokuwa wanasumbulia na adhaa ya ukosefu wa maji.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso wakati akizungumza na wananchi wa Seluka katika mkutano wa hadhara. Ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kubeba lita 100,000 unatarajia kugharimu Zaidi ya Million 45.
“Maneno matupu katika Wizara yetu ya Maji hatuyataki, tunataka wananchi wetu wapate maji ili dhamira ya Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan iweze kutekelezeka,” alisema Waziri.
Waziri ametoa muda wa siku 30 kwa RUWASA kurekebisha miundo chakavu ya maji katika vijiji vya Seluka Nyabu na Wihenzele uwe umekamilika na maji yaanze kutoka.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Mb) wa Kibakwe Mhe. George Simbachawene amesema 2004-2005 serikali ilitoa millioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya maji: mtandao wa maji ukawekwa na pampu ya maji inayotumia dizeli ikawekwa sambamba na tenki la maji kujengwa lakini bado wananchi hawakupata maji.
“Tulipata milioni 157 ya ukarabati wa miundombinu ya maji kwa ajili ya kurekebisha kisima cha maji na maeneo mabovu ambayo kazi hiyo ilifanyika. Katika kufufua kisima cha maji kinachotumia diesel, ilitokea changamoto ya kukosekana uwiano mzuri kati ya kiwango cha maji kinachopandishwa na uwezo wa jereta, ambayo nayo ilianza kusumbua”
Naye Bi. Easter Mgonela Mkazi wa kijiji cha Seluka amesema shida ya maji imesababisha ukatili wa kijinsia, ameomba serikali kutatua changamoto ya kukosekana maji haraka.